NI KAULI YAKE MKUU WA MKOA WA DAR ES SALAAM MH PAUL MAKONDA KUELEKEA TAREHE 09/04/2018 SIKU ALIYOITANGAZA YA KUSIKILIZA KERO ZA WAKINAMAMA WALIOTELEKEZWA NA WAUME ZAO MKOANI KWAKE.
Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Mh Paul Makonda amewataka wanawake wote waliotelekezwa na waume zao kufika ofisini kwake tarehe 09/04/2018 ili kuweza kusikilizwa matatizo yao na kupatiwa ufumbuzi kwa mujibu wa sheria.
Ameitoa kauli hiyo leo alipokuwa akiongea na wanawake wa Mkoa wa Dar es Salaam katika sherehe ya siku ya wanawake duniani yenye kauli mbiu isemayo "Kuelekea uchumi wa viwanda, tuimarishe usawa wa jinsia na uwezeshaji wa wanawake vijijini "
Amesema katika Mkoa wake amebaini wanawake wengi kutelekezwa na waume zao na hivyo kufanya idadi kubwa ya watoto kulelewa na mzazi mmoja, na wengine kuua vichanga vyao na wengine kuwatupa watoto hali inayopelekea kuwa na watoto wengi wa mtaani.
"Nimebaini wakinababa wengi wamewatelekeza wakinamama, wamewapa ujauzito na kuwaacha wakawafanya wakinamama kutoa mimba, wakawafanya wakinamama kuua vichanga vyao, wakawafanya wadada wengi kufukuzwa majumbani kwao, wakati wao wamekaa wakistarehe pasipo kujali. ..sasa kinamama hamtateseka wala hamtadai fedha za matumizi peke yenu nitakua nanyi kuhakikisha mnapata fedha za hizo "Amesema Makonda
Ameongeza kuwa kwa mujibu wa sheria ya mwaka 2009 iliyotungwa inayozungumnzia haki ya mtoto inamtaja baba moja kwa moja kama mlezi wa kwanza akishirikiana na Mama katika malezi ya mtoto.
Maadhimisho haya ya siku ya wanawake yaliyofanyika kimkoa katika ukumbi wa Mlimani city pamoja na viongozi wa vyama na Serikali, pia yamehudhuriwa na vikundi mbalimbali vya wajasiriamali kutoka Manispaa ya Kinondoni, Ilala, Temeke, Kigamboni na Ubungo.
Imetolewa na
Kitengo cha Habari na Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.