Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mh Paul Makonda amezindua rasmi ujenzi wa jengo la utawala katika shule ya Sekondari Makumbusho linalofadhiliwa na China ikiwa ni muendelezo wa Majengo 402 ya utawala yanayotarajiwa kujengwa Mkoa wa Dar es salaam nje ya bajeti ya Serikali.
Uzinduzi huo umefanyika leo katika shule ya sekondari Makumbusho hafla iliyohudhuriwa na walimu wakuu wa Shule za sekondari, wakuu wa idara na vitengo Manispaa ya Kinondoni ,Wazazi, pamoja na wanafunzi wa Shule ya sekondari Makumbusho.
Akiongea katika uzinduzi huo Mh Makonda amesema wakati umefika sasa wa Serikali kutambua thamani ya mwalimu kwa vitendo na uungwana kwa kuhakikisha wanapatiwa mazingira mazuri na ya kuridhisha kwani wao ndio nguzo kubwa ya mafanikio kuelekea uchumi wa viwanda.
"Tambueni thamani ya mwalimu inatokana na vitendo na uungwana, tunahangaikia moyo wa Uchumi wa watanzania " amebainisha Makonda
Naye balozi wa China nchini Tanzania Bibi Wang Ke amesema Kuwa Serikali ya China iko bega kwa bega katika kuunga mkono juhudi za serikali ya Tanzania za kuboresha mazingira ya waalimu .
Kadhalika ameongeza kuwa China wanaamini katika kuwekeza kwenye Elimu kwani yaweza kubadilisha maisha ya watu na kuongeza wataalamu watakaoleta maendeleo nchini.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Makumbusho katika taarifa yake Bi Edna Ngeregeza ameainisha changamoto za shuleni hapo kuwa ni uhaba wa vyumba vya madarasa, upungufu wa waalimu wa masomo ya Sayansi na biashara pamoja na uzio wa shule.
Jengo hilo la utawala linatarajiwa kukamilika ndani ya miezi mitatu kuanzia Sasa na litasaidia kupunguza tatizo la upungufu wa madarasa shuleni hapo kwani kwa hivi Sasa vyumba 4 vya madarasa vinatumika Kama ofisi za walimu.
Imetolewa na
Kitengo Cha Habari na Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.