NI KUFUATIA MRADI WA KUBORESHA MAZINGIRA YA WAALIMU WA MKOA WA DAR ES SALAAM NJE YA BAJETI YA SERIKALI WENYE LENGO LA KUJENGA MAJENGO 402 YA UTAWALA.
Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Mh Paul Makonda amezindua zoezi la uezekaji wa mabati juu ya jengo moja kati ya majengo 46 ya utawala yanayoendelea kukamilika katika mradi wa majengo 100 yanayojengwa kwa wakati mmoja kwa lengo la kuboresha Mazingira ya waalimu nje ya bajeti ya Serikali kwa shule za Msingi na Sekondari.
Uzinduzi huo umefanyika leo katika shule ya msingi Mapinduzi iliyoko Kata ya Kigogo kwa kuweka mabati sita kwenye jengo la utawala hafla iliyohudhuriwa na viongozi wa chamá na Serikali, Wah Madiwani, Wakuu wa Idara na vitengo wa Halmashauri za Mkoa wa Dar Es Salaam pamoja na Wadau wa Elimu.
Amesema kwa kuweka bati jengo hilo ni kuelekea kwenye hatua za mafanikio zinazoleta matokeo chanya katika sekta ya Elimu kwa kuhakikisha Mazingira yanaboreshwa kwa kiwango kinachokubalika na chenye ubora na hasa ikizingatiwa lengo ni kujenga Majengo 402 kwa shule za Msingi na Sekondari Mkoani Kwake.
"Ili si Jambo rahisi, na hata wakati tunaliwaza wengi walisema haliwezekani, na wengine wakabaki kuuliza idadi ya ofisi, wanapotajiwa ni idadi ya ofisi 402 wanasema hili Jambo haliwezekani, leo ninaposimama mbele yenu si tu kwamba tunaongelea mapango, si tu kwamba tunaongelea ufyatuaji wa matofali, si tu kwamba tunaongelea ujenzi wa msingi, bali sasa tunaongelea uwekaji wa bati juu ya jengo moja kati ya majengo 46 yanayoendelea kukamilika kwenye mradi wa majengo 100 kwa wakati mmoja " Amebainisha Mh Makonda.
Ameongeza kuwa mradi huu unaendeshwa na wananchi wenyewe ikiwa ni katika kumuunga mkono Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Joseph Magufuli katika dhamira yake timilifu ya kutoa elimu bure kwa wanafunzi kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha nne.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Mh Benjamin Sitta amempongeza Mh Makonda kwa ubunifu na juhudi alizonazo za kuboresha mazingira ya waalimu na Elimu na kumuunga mkono kwa kuiomba kamati ya ujenzi ya Mkoa kupeleka wajenzi kwenye shule nne za Manispaa hiyo ambazo tayari zina vifaa vyote vinavyotakiwa hadi kukamilika kwake
Amezitaja shule hizo kuwa ni shule ya Msasani B, shule ya kyumbageni iliyoko mbweni, shule ya ununio iliyoko kunduchi, na Shule ya Mtongani iliyoko kunduchi.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Mapinduzi Bi Fina Mauky amezitaja changamoto za shule yake katika risala aliyoisoma kwa Mkuu wa Mkoa kuwa ni kuvamiwa kwa mipaka ya shule, ukosefu wa uzio kunakosababisha vibaka kupora vifaa vya wanafunzi na raia wapitao kwa miguu kukabwa nyakati za usiku.
Akizijibu changamoto zilizotolewa na uongozi wa shule hiyo Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wavamizi wa maeneo ya shule kuchukuliwa hatua za kisheria, na Maafisa Mipangomiji wa Halmashauri za Mkoa wa Dar Es Salaam kuhakikisha wanafufua mipaka ya shule zote zilizovamiwa katika Halmashauri zao.
Imetolewa na
Kitengo cha Habari na Uhusiano.
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.