MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Amos Makalla leo tarehe 11 Novemba, 2021 amezindua mradi wa soko wenye lengo la kuwawezesha wafanyabiashara wadogo kujikwamua kiuchumi, katika eneo la Kigogo, mradi ambao umetekelezwa na kampuni ya Coca-Cola Kwanza Ltd kama sehemu ya kuchangamana na jamii kwa kurudisha fadhila.
Makalla ameishukuru Kampuni ya Coca-Cola Kwanza kwa kuwezesha mradi huo utakaowawezesha wajasiriamali zaidi ya 100 kufanya biashara zao kwenye eneo rasmi na kuwaasa wafanyabiashara kuchangamkia fursa mbalimbali za biashara katika soko hilo.
Awali Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam iliainisha maeneo ambayo wafanyabiashara wadogo maarufu kwa jina la Machinga wanatakiwa kuondoka kuwa ni kwa wale walio juu ya mifereji na mitaro, kwenye hifadhi za barabara na mbele ya shule za Serikali au taasisi za Serikali.
Maeneo mengine wasiotakiwa kuwepo wafanyabiashara hao ni njia za waenda kwa miguu na wale waliopo mbele ya biashara za maduka ya watu.
“Wafanyabiashara wadogo waliorudi kwenye maeneo waliyotolewa, niwaombe mrudi kwenye maeneo mliopangiwa kufanya biashara zenu, kwa sababu zoezi la kuwapanga ni endelevu kwa mkoa wote wa Dar es Salaam”, ameeleza Makalla.
Kampuni ya Coca-Cola Kwanza imewezesha ujenzi wa soko la kisasa la Kigogo lenye miundombinu bora ili kuwawezesha vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kufanya biashara katika eneo rasmi na kuweza kujikwamua kiuchumi.
RC Makalla amesema ataomba Mamlaka husika kuelekeza mabasi ya abiria maarufu Daladala kutumia njia hiyo kama Kituo chao ili kuchangamsha eneo hilo kibiashara.
Hafla hiyo ya kukabidhi na kuzindua mradi wa soko la Kigogo imehushuhudiwa na wajumbe wa Kamati ya Fedha na Uongozi ya Manispaa ya Kinondoni ikiongozwa na Mstahiki Meya wa Manispaa Mheshimiwa Songoro Mnyonge, Menejimenti ya Manispaa ya Kinondoni chini ya Kaimu Mkurugenzi ndugu Shadrack Maximilian, uongozi wa kampuni ya Coca-Cola Kwanza ukiongozwa na Meneja Mtendaji, Unguu Sulay pamoja na wananchi na viongozi mbalimbali wa Kata ya Kigogo.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.