Rai hiyo imetolewa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, jinsia wazee na watoto Mhe. Ummy Mwalimu katika ziara yake Manispaa ya Kinondoni kwa lengo la kushiriki zoezi la unyunyuziaji wa viuadudu (biolarvicides) kwa mazalia ya mbu ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono zoezi la uhamasishaji wa udhibiti wa ugonjwa huo katika Wilaya hiyo.
Amesema swala la uwajibikaji udhibiti wa mazalia haya ya mbu ni ya kila mwananchi, kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia si tu kuondokana na ugonjwa wa Dengue, bali pia magonjwa mengine kama vile Malaria, zika, matende, Atikungunya na homa ya manjano.
Amesema "Kwanza niipongeze Manispaa ya Kinondoni kwa kuonesha jitihada za kuhakikisha wanadhibiti ugonjwa huu wa Dengue kwa kununua mashine na viuadudu hivi ambavyo leo tunapulizia dawa, katika kupambana na mazalia ya mbu lakini pia niwapongeze kwa kupunguza idadi ya wagonjwa wapya wa homa ya Dengue kutoka 45 kwa siku mwezi April mpaka kufikia wagonjwa 17 kwa siku mwezi June" Waziri Ummy.
Naye Mkuu wa wilaya ya Kinondoni Mhe Daniel Chongolo amesema Kinondoni imeshafikia asilimia 70 ya maeneo yake kwa kupulizia dawa ya kuua mazalia ya mbu kwa kutumia vikundi vya jamii vinavyopita mtaani na kubainisha hatua ambazo tayari zimeshakuliwa kuendelea kudhibiti mazalia haya ya mbu ambayo ni uagizaji wa mashine maalum za upuliziaji hewani (Fog machine) ambazo zitawezesha kupuliza dawa eneo kubwa zaidi kwa muda mchache.
Aidha Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni Dkt Festo Dugange katika nafasi yake amewataka wananchi mara waonapo dalili za homa ya dengue kuwahi kituo cha afya ili waweze kupata matibabu stahiki na kuachana na tiba za mtaani kama majani ya mpapai na mafuta ya nazi.
Zoezi hilo la upuliziaji viuadudu vya kuua mazalia ya mbu limehudhuriwa pia na Mbunge wa Kinondoni Mh Maulid Mtulia, Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Mhe. Benjamin Sitta, Mkurugenzi wa Manispaa Ndg Aron Kagurumjuli na wakazi wa Eneo la Mwananyamala.
Imeandaliwa na
Kitengo Cha Habari na Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.