Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini zimetakiwa kupunguza matumizi ya karatasi na badala yake kuimarisha mifumo ya TEHAMA katika utekelezaji wa kazi za kila siku.
Wito huo umetolewa leo na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Laurean Ndumbaro, wakati wa ufunguzi wa Kikao kazi cha tatu cha Serikali Mtandao.
Kikao kazi hicho cha siku tatu kinafanyika Ukumbi wa AICC, Arusha kimejumuisha Viongozi Watendaji Wakuu wa Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Mashirika ya Umma na Sekta Binafsi.
Dkt. Ndumbaro amesema, "tuanze katika ofisi zetu, tupunguze matumizi ya karatasi na shughuli ziwe za kidigitali. Vikao vya Menejimenti na Mabaraza ya Madiwani viwe vya kidigitali."
Aidha, Dkt. Ndumbaro aliwakumbusha washiriki wa kikao kazi hicho kuhuisha taarifa zao zilizoko kwenye Tovuti na ziendane na wakati.
"Tubadilishe Tovuti zetu ziwe za kisasa na taarifa zake ziendane na wakati. Pia, tumieni vishikwambi na tuimarishe mifumo yetu," Alisema.
Katika kutekeleza maelekezo hayo, Manispaa ya Kinondoni imekuwa ni Manispaa ya kwanza nchini inayotumia Mfumo wa Ofisi Mtandao "e-office" katika shughuli zake za kila siku.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Bi. Hanifa Suleiman Hamza, mara kwa mara amekuwa akisisitiza matumizi ya TEHAMA kwa lengo la kurahisisha utoaji wa huduma na kupunguza matumizi ya karatasi.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.