Na Songoro Mnyonge, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni.
Umetangulia mbele ya haki na kutuachia majonzi. Mapenzi yake Maanani yametimia. Inna lilahi wa inna ilayhi rajioon. Tangulia Mzee tutakukumbuka kwa mengi. Rais wa Awamu ya Pili uliyeifungua nchi zama hizo!
Tulikwita Mzee Rukhsa kwa sababu ya ukarimu wako. Hukutaka mtu aonewe kisa utashi wa nafsi yake, aliyetaka kula chura ale, hiyo ilikuwa kauli yako! Nchi ukaifungua na uchumi wa kila raia kuimarika.
Kila mmoja alipambania maisha yake pasi na kuvunja sheria. Hiyo ndio maana ya Rukhsa uliokuwa umeitaka na umeiishi hadi Mwenyezi Mungu alipokuita.
Licha ya kustaafu Urais uliendelea kuwa Mnyenyekevu, mpole, mwenye upendo na Mstahamilivu. Ulimpenda kila mmoja, mkubwa hadi mdogo.
Uliipenda dini yako na katu hukuisaliti na leo umeondoka ukiwa unaishadidiya bila kubagua dini wala madhehebu ya wengine. Wewe ndiye Mzee Rukhsa tunayekulilia.
Ulipokuwa umepumzika, hukukasirika tulipokugongea na shida zetu kukueleza na kwa moyo mmoja ukatutimizia.
Kinondoni Manispaa yako, hukuitupa mkono, Yusuph Mwenda akiwa Meya wa miaka hiyo na mimi nikiwa Naibu wake hukuchoka kutusikiliza na kutusaidia pia. Tulikutaka uje kututembelea wanao na kweli ulikuja na mawaidha kutupatia. Na leo tupo tulipo ni kwa kufuata nyayo na mafunzo yako.
Wana Kinondoni wanakulilia wakiwemo vijana wa KMC FC ambao wewe ndiye uliyewazindulia jezi tulipoanzisha timu miaka 14 iliopita. Tangulia Mzee wetu na tunamwomba Mola akupokee na kukuhifadhi mahala pema peponi- Amein
Mwandishi wa shahiri hili ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Mheshimiwa Songoro Mnyonge.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.