Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi leo Jumatatu tarehe 12 Disemba, 2022 amekutana na Watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni katika kikao kazi cha kusikiliza kero/malalamiko/changamoto za watumishi kilichofanyika katika ukumbi wa shule ya Sekondari Turiani, uliopo Kata ya Ndugumbi Manispaa ya Kinondoni.Katika kikao hicho Watumishi walipata fursa ya kuelezea changamoto za kiutumishi na kupatiwa ufafanuzi hususani katika maeneo yanayohusu kupandishwa madaraja, kubadilishwa vyeo, madai ya nyongeza za mishahara na malimbizo ya mishahara na yaliyojibiwa vizuri na Naibu Waziri sambamba na kutolea ufafanuzi na kukidhi kiu ya Watumishi.
Akizungumza wakati wa majumuisho ya kikao hicho aliwataka Watumishi wote kutekeleza kwa ufanisi majukumu yao kwa kutoa huduma bora kwa wanachi na kwa wakati kwani Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonyesha mapenzi makubwa kwa watumishi wa umma kwa kulipa malimbikizo ya mishahara kwa watumishi wa Kinondoni kutoka Milioni 313 hadi Bilioni 1.7 na kupandisha madaraja watumishi 1,276 katika kipindi kifupi cha utawala wake hivyo amewataka watumishi kuthamini adhima hiyo ya Rais kwa kufanya kazi kwa uhakika, bidii na ufanisi wa kiwango cha juu.
Mhe. Ndejembi amewakumbusha watumishi masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuacha ukirimba, kuacha majungu, usengenyaji kazini, na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.
Pia alisisitiza umuhimu wa kila mtumishi wa umma kuwa na mpango kazi wa siku, wiki, mwezi na mwaka katika kutoa huduma kwa wananchi utakaowezesha kujitathimini binafsi na kuwaagiza Wakuu wa Divisheni na Vitengo kukutana na watumishi walio chini yao na kusikiliza kero hasa Divisheni ya Utumishi na Utawala.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Kinondoni Bi. Stella Msofe, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni Mhe. Songoro Mnyonge na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni Bi. Hanifa Sulemani Hamza ambapo walimshukuru Naibu Waziri kwa kutenga muda wake kuzungumza na watumishi hao na kumuahidi usimamizi wa karibu kutoka kwao katika kutekeleza maagizo yote aliyotoa katika kikao hicho.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini:
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.