APEWA MWEZI MMOJA KULIPA DENI LA TSH 99 MILIONI ANALODAIWA NA MANISPAA.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh Ali Hapi amemtaka mwekezaji wa kituo cha makumbusho kuacha mara moja kutoza wamachinga wa kituo hicho fedha zisizo ndani ya mkataba wake wa uwekezaji
Amelitoa agizo hilo leo alipokuwa katika ziara yake ya Kiserikali katika soko la Makumbusho kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero za wananchi ambapo alipata nafasi ya kuongea na wafanyabiashara pamoja na Mama lishe wa sokoni hapo.
Amesema kwa kufanya hivyo ni dhuluma, na ni uonevu pia ni kinyume cha sheria kwa mtu yeyote yule kufanya mambo yaliyo nje ya mkataba wowote ule.
"Mwekezaji kuanzia leo ni marufuku kutoza fedha ulizokuwa unawatoza vijana wa bajaji, fedha ambazo haziko kwenye mkataba, malipo yeyote ambayo hayako kwenye mkataba hana haki ya kutoza malipo hayo "alisisitiza Hapi
Ameongeza kuwa ni vema mkataba huo ukapitiwa upya ili kuona kama unatija au la ili hatua stahiki zichukuliwe kwa maslahi ya Taifa.
Alipotakiwa kutoa ufafanuzi kuhusiana na deni Mwekezaji huyo analodaiwa na Manispaa Bw. Dismas Hafidhi ambaye ni Meneja wa vituo vya Mabasi Manispaa ya Kinondoni . amesema mwekezaji huyo ajulikanae kwa jina la Estern Capital anadaiwa kiasi cha tsh 99Milioni.
Hata hivyo mwekezaji huyo alipotakiwa kuthibitisha deni hilo alikiri kudaiwa kiasi hicho na kuahidi kulilipa ndani ya muda uliopangwa.
Katika hatua nyingine Afisa Masoko wa Manispaa hiyo Bw. Zahoro Hanuna ametakiwa kusimamia Sheria, kanuni na taratibu zinazotakiwa za kuendesha masoko ili kuepukana na migogoro isiyoyalazima hasa ile ya mtu mmoja kumiliki kizimba zaidi ya kimoja.
Aidha ametakiwa kuhakikisha magenge yote yaliyoko kwenye maeneo ya Masoko yanaondolewa.
Imetolewa na
Kitengo cha Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.