Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Saad Mtambule amezindua rasmi zoezi la upimaji wa afya bure kwa wananchi wa Wilaya ya Kinondoni.
Zoezi hilo la upimaji wa afya bure limezinduliwa leo Julai 16, 2023 katika viwanja vya CCM Mwinjuma vilivyopo Kata ya Makumbusho likiwa na lengo la kuwasaidia wananchi kupata huduma za afya bila malipo pamoja na kuwajengea tabia ya kupima afya zao mara kwa mara.
“Niwaombe wananchi wote wa Kinondoni kujitokeza na kutumia fursa hii ya kupima afya zetu na kupata matibabu bure na kwa muda mfupi kwani ukitumia utaratibu wa kawaida ni gharama na inachukua muda mrefu sana hivyo tujitokeze kwa wingi katika kupima ili tujue afya zetu,” amesema Mhe. Mtambule.
Pia Mhe. Mtambule amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa maelekezo mazuri ya usimamizi wa upimaji afya bure kwa wananchi wa Kinondoni na Mkoa wa Dar es Salaam kwa ujumla.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni Mhe. Songoro Mnyonge ametoa wito kwa wananchi wa Manispaa ya Kinondoni kujitokeza kwa wingi katika kupima afya zao.
Aidha, Mhe. Songoro amesema kuwa zoezi hilo lina faida kubwa kwa wananchi wa Kinondoni kwani mbali na upimaji afya zao lakini pia watapata ushauri juu ya magonjwa ya moyo na mifupa kutoka taasisi ya Jakaya Kikwete (JKCI) na MOI.
Nae Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Dkt. Samwel Laizer amesema lengo la zoezi hilo ni kusaidia wananchi kujenga tabia ya kuchunguza afya zao kwani Watanzania wengi hawana tabia ya kwenda kuchunguza afya zao mara kwa mara.
Lakini pia Mganga Mkuu huyo amesema katika zoezi hilo wanatarajia kuwahudumia wananchi zaidi ya 4,000.
Ikumbukwe kuwa zoezi hilo limeratibiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila, kutoa huduma za upimaji wa afya bure kwa muda wa siku kumi katika Wilaya zote 5 za Mkoa huo ambapo kila Wilaya itatoa huduma ya upimaji kwa muda wa siku 2.
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini: Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.