NI ULE UHUSIANAO NA JINSI YA KUJIZUIA NA KUJIKINGA NA MAAMBUKIZI YA MAGONJWA KWA KUNAWA MIKONO KWA USAHIHI.
Mradi uliofadhiliwa na shirika lisilo la kiserikali la Japan international Cooperation Agency (JICA), juu ya kujizuia na kujikinga na maambukizi ya magonjwa kwa kunawa mikono kwa usahihi wafikia tamati.
Hitimisho hilo limefanyika leo katika shule ya Msingi Kigogo ambapo Mgeni rasmi katika shughuli hiyo ni Afisa Afya wa Manispaa Ndg John Kijumbe hafla iliyohudhuriwa na wageni kutoka Jica, Maafisa Kutoka Manispaa, pamoja na wanafunzi ambao ndio walengwa wakubwa.
Akizungumnzia mradi huo Ndg Kijumbe amesema pamoja na vitu vingine umeleta mafanikio makubwa yakiwemo kupungua kwa magonjwa yatokanayo na mikono michafu, kukuza uelewa juu ya elimu iliyotolewa kuhusiana na kunawa mikono, pamoja na usambazaji wa vifaa vya kunawia mikono mashuleni.
Aidha amebainisha changamoto zilizojitokeza wakati wa kuratibu mradi huo kuwa ni somo la kuzuia na kujikinga na maambukizi ya magonjwa kwa kutokunawa mikono kwa usahihi kutokuwa katika mitaala ya shule pamoja na ufinyu wa bajeti katika mpango kazi wa Halmashauri unaopelekea kushindwa Kuendeleza zoezi la unawaji mikono kwa usahihi.
Naye Mganga mfawidhi wa Kituo cha Afya Magomeni Dr. Omary Mwangaza amesema maradhi mengi yanayowapata watoto chini ya miaka mitano ni kutokana na kutumia mikono yao ikiwa michafu.
Ameongeza kuwa ni vema swala la kunawa mikono likawa sehemu ya mila na desturi ya wazazi kuwafundisha watoto, kwani kwa kufanya hivyo kutaisaidia serikali kupunguza bajeti kubwa inayopelekwa kwa matibabu ya watoto na kufanya vitu vingine vya Maendeleo.
Akiwashukuru Shirika la JICA kwa mradi huo, Afisa Afya kituo cha Magomeni ambaye ni mratibu wa mradi huo ameyataja maeneo ambayo mradi umetekelezwa kuwa ni Kata ya Tandale, Kigogo na Magomeni.
Aidha ameainisha mapendekezo yanayohitajika ili kuendelea kutekeleza mradi huo kuwa ni kutenga bajeti ya kutosha, kuwepo na muendelezo wa kufundisha wanafunzi juu ya maswala ya kunawa mikono, kuimarisha ushirikiano kati ya Nchi ya Japan na Tanzania, na kuwepo mtaala wa kufundishia mashuleni unaohusu njia kumi za unawaji mikono kwa usahihi.
Imetolewa na
Kitengo cha Uhusiano na Habari.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.