Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kwa kushirikiana na Wataalamu wa ardhi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo cha Ardhi Machi 18, 2024 wamekutana na kujadili mpango wa kuboresha Mpango wa matumizi ya ardhi wa Oysterbay na Masaki ili kuendana na mahitaji ya sasa.
Akifungua kikao cha pili cha majadiliano hayo (Oysterbay Masaki Development Scheme) baina ya Kamati ya Wataalam hao na Wakuu wa Idara na Vitengo vya Manispaa ya Kinondoni, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Mheshimiwa Songoro Mnyonge, alisema kuwa mpango unaoendelea kutumika sasa ulipitishwa Mwaka 2008, ambapo umekumbwa na baadhi ya changamoto katika utekelezaji wake zinazotokana na mahitaji makubwa kuliko mpango wenyewe.
"Ardhi ya Oysterbay na Masaki ina thamani kubwa, baadhi ya watu wanajenga nje ya utaratibu. Pia panageuka kuwa eneo la kibiashara, ipo haja sasa ya kufanya marejeo ya Mpango wa sasa wa uendelezaji ili uendane na mahitaji halisi."
Baadhi ya matumizi ya eneo la hekta 800.6 linalopendekezwa kuboreshewa matumizi ya ardhi ni Biashara kutoka asilimia 0.4 hadi 11.3; Makazi kutoka asilimia 74.3 hadi 40.8; Taasisi kutoka asilimia 1.2 hadi 12.5 na Makazi na biashara kutoka asilimia 5.4 hadi 16.8.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Ardhi, Bi. Ramla Ahmed, alisema mpango huo tarajiwa utakuwa na faida kubwa kwa Manispaa ya Kinondoni na Mkoa wa Dar es Salaam kwa ujumla kwani Mkoa huu umeendelea kuwa Mji wa Kibiashara.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.