Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh Alli Hapi amezindua mtandao wa tasnia ya wafugaji wa Ng'ombe wa maziwa Wilaya ya Kinondoni wenye lengo la kuwarahisishia upatikanaji wa fursa mbalimbali zitolewazo na Serikali kwa mfumo wa vikundi kama vile mikopo.
Uzinduzi huo umefanyika leo katika ukumbi wa COSTECH jijini Dar es Salaam ambapo vikundi zaidi ya 13 vyenye wanachama zaidi ya 200 vimeshiriki.
Akiongea Mara baada ya uzinduzi huo Mh Hapi amesema wafugaji wengi wanatakiwa kuhakikisha wanajiunga kwenye vikundi kwani ndio njia rahisi na pekee ya wao kufaidika na huduma mbalimbali zitolewazo na Serikali.
Amezitaja huduma hizo kuwa ni mikopo, mafunzo juu ya elimu ya ufugaji wa kisasa utakaowajengea uwezo, urahisi wa upatikanaji wa tarifa zinazowahusu pamoja na jinsi ya kupata masoko ya uhakika.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo ambaye pia ni Mkuu wa idara ya Mifugo Bi Patricia Henjewele amesema kuwa kwa Wafugaji wa Ngo'mbe wa maziwa kujiunga kwenye vikundi itawarahisishia Serikali kupeleka misaada ya wataalam kwa ajili ya kutoa elimu sahihi ya ufugaji wa kisasa na jinsi ya kupata matokeo mazuri ya mazao ya maziwa.
Katika hatua nyingine Mh Hapi ametoa rai kwa watanzania kujenga mazoea ya kunywa maziwa kwa lengo la kuimarisha afya ya mwili kunakoenda sambamba na virutubisho muhimu vinavyopatikana kwenye maziwa.
" Ndugu zangu sekta ya maziwa ni Moja katika sekta nyeti na muhimu Sana kwa ukuaji na afya zetu Kama binaadamu, hivyo nasisitiza tujenge mazoea ya kunywa maziwa kwa ajili ya kuboresha afya zetu" Amesisitiza Hapi
Awali akitoa taarifa mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mwenyekiti wa mtandao huo wa maziwa Bw Nyaupe ameushukuru uongozi wa Manispaa ya Kinondoni kuzindua mtandao huo kwani wafugaji wakiwa pamoja inakuwa rahisi kupata fursa ya kubadilishana uzoefu wa kitaalam na kupeana miongozo ya masoko itakayowasaidia kufanikiwa katika shughuli zao.
Imetolewa na
Kitengo cha Uhusiano na Habari
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.