Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh Ali Hapi ametoa siku kumi na nne kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Kawe kuhakikisha wafanyabiashara wa Bunju wanaofanya biashara barabarani kuhamia sokoni.
Amelitoa agizo hilo leo alipokuwa akihutubia katika mkutano wa hadhara uliohusisha wafanyabiashara wa Bunju katika viwanja vya Bunju B vilivyoko kata ya Mabwepande Manispaa ya Kinondoni.
Amesema viongozi wa soko wakutane na uongozi pamoja na mamlaka husika wakae, wafanye mazungumnzo, wapange mikakati na kufikia makubaliano ya kutekeleza agizo alilolitoa ndani ya muda.
"Hayo ndio maelekezo ya Serikali ya Wilaya ninayoiongoza, na haya ndio maelekezo ya Rais wetu mpendwa Dr John Pombe Magufuli ambayo sisi tunayatekeleza, asitokee mtu hata mmoja kurefusha siku hizo Kati ya siku nilizozitoa "amesema Hapi.
Ameongeza kuwa kwa mtu yeyote kuendelea kufanya biashara barabarani ni kinyume cha sheria, na pia ni kuhatarisha maisha yako mwenyewe.
Aidha amezitaka mamlaka husika kuhakikisha sheria Zinafuatwa na kufikia siku ya kumi na nne eneo la hifadhi ya barabara linakuwa jeupe.
Katika hatua nyingine amewataka Maafisa watendaji wa Kata kutozuia Mwananchi yeyote kupata eneo la kufanya biashara katika Masoko yaliyopo Manispaa ilimradi ni mkazi wa Kinondoni.
"Ni marufuku kwa Mwananchi yeyote kuzuiwa kwenda kupata nafasi kwenye eneo la soko, ilimradi awe ni Mwananchi wa Kinondoni, na wa eneo hilo, Kata hiyo, aende asinyimwe nafasi "aliongeza Hapi.
Leo ni siku ya Pili, kati ya siku nne ambazo Mkuu huyo wa Wilaya anatarajia kufanya ziara ya kikazi kwenye Wilaya yake.
Imetolewa na
Kitengo cha Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.