Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Mhe Paul Makonda leo amefanya ziara katika wilaya ya Kinondoni kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa fedha kutoka serikali kuu ,Mapato ya ndani ya Manispaa na fedha za wadau wa nje na ndani ili kujiridhisha kwa kulinganisha taarifa anazopewa na hali halisi katika maeneo ya mradi husika ambapo pamoja na kupongeza hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa Miradi hiyo ametoa Maagizo na maelekezo mbalimbali yanayotakiwa kufanyiwa kazi ili kuboresha na kuifanya iendane na thamani halisi.
Katika mradi wa ujenzi wa soko la magomeni Mhe. Mkuu wa mkoa alionesha kutoridhishwa na ubadilishaji wa dizaini ya ujenzi wa Soko hilo, hivyo amewataka Wahandisi na Wataalam wengine wanaosimamia Miradi mbalimbali ya ujenzi kutokubali Wahandisi washauri wa miradi kubadilisha dizaini ya miradi hiyo, kwani inaweza kupoteza ubora na kutoa huduma kwa wachache tofauti na lengo la serikali la kuangalia mahitaji ya sasa na baadae.
Akiwa katika kituo cha Afya Kigogo, Mhe.Mkuu wa Mkoa pamoja na kuupongeza uongozi wa wa Manispaa ya Kinondoni kwa maamuzi ya busara ya kununua majengo, kuyakarabati na kujenga majengo mengine kwa matumizi ya Kituo kikubwa cha Afya kitakachohudumia zaidi ya wakazi laki moja, ameagiza kasi ya utekelezaji wake iongezwe na endapo kutakuwa na jambo linalokwamisha kuhusiana na ufuatiliaji katika Mamlaka za juu ashirikishwe Mkuu wa Wilaya kwani heshima ya Serikali kutaka kupata matokeo ya Mradi kwa wakati na sio ugumu wa kupata matokeo ya miradi inayotekelezwa.
Mhe Mkuu wa mkoa alieleza kutoridhishwa na baadhi ya Barabara zinazojengwa chini ya kiwango hususani Barabara ya Mburahati ambapo pamoja na Mkandarasi kuwa nyuma ya muda wa Utekelezaji, viwango vya ubora wake sio wa kuridhisha katika upana na ubora wa mifereji ya maji ya mvua, hivyo amewataka wasimamizi wa mradi huo kuhakikisha wanafanyia kazi ili kuiwezesha kuwa katika viwango vinavyokubalika.
Akizungumzia gharama za ujenzi wa miradi ya barabra hizo, Mhe. Mkuu wa Mkoa amezitaka Mamlaka husika kuliangalia suala la tofauti ya gharama za ujenzi kwa Miradi ya Barabara ya DMDP inayojengwa kwa thamani ya bilioni 2 kwa kilometa moja na zile za TANROAD na TARURA zikijengwa kwa thamani ya bilioni 1.3 kwa kilometa moja, kwani tofauti ni kubwa na fedha zinazotumika katika ujenzi ni mkopo sio msaada, hivyo akashauri kuliangalia jambo hili.
Katika hatua nyingine Mhe. Mkuu wa Mkoa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Daniel Chongolo kushughulikia malalamiko ya vibarua wanaodai kupunjwa malipo yao na kampuni za ujenzi ambazo huwalipa shilingi 7500 kwa siku badala ya shilingi 12,500 kwa siku zinazotakiwa kulipwa kisheria.
Katika hatua nyingine Mhe. Mkuu wa Mkoa ameshauri Fedha zilizotakiwa kutumika katika ujenzi wa kipande cha mita 200 katika Barabara ya Simu 2000 na nyingine zikajenge Barabara ya Shekilango Ubungo maziwa kupita Makaburi ya Urafiki ili kuondoa kero kwa watumiaji wa Barabara hiyo.
Akiwa katika Mradi wa ujenzi wa soko la Sinza II Kata ya kijitonyama ambapo linajengwa kwa gharama ya milioni 128 zinazotokana na mapato ya ndani ya Manispaa, Mhe. Mkuu wa Mkoa amefurahishwa na Ubora wake na kutaka likamilishwe haraka na kuwaweka wafanyabiashara sambamba na kuboresha maeneo ya maegesho na njia ya kuingilia Magari Sokoni hapo.
Aidha katika ziara hiyo Mhe Mkuu wa Mkoa alionesha kusikitishwa kwake na baadhi ya maeneo kuwa na mazingira machafu hivyo ameuagiza uongozi wa Manispaa kuhakikisha Maafisa Watendaji wa Kata katika maeneneo hayo kuanza kujitathmini uwezo wao katika kusimamia usafi kwani kama Watendaji Wakuu wa Maeneo husika wana wajibu wa kuwasimamia Maafisa Afya wa Kata kutekeleza kikamilifu Majukumu yao.
Mwisho Mhe. Mkuu wa Mkoa amewataka wakandarasi wa Kampuni ya Scoll na Del-monte waliosimamishwa kupewa miradi ya ujenzi katika Mkoa wa Dar es salaam kwa kosa la kujenga Barabra chini ya kiwango, kuzijenga upya kwa gharama zao kama walivyoagizwa haraka iwezekanavyo ili waweze kupewa miradi mingine ambapo amempongeza Mkandarasi wa kampuni ya Delmonte anayerudia ujenzi katika barabara ya Mabatini kwa gharama zake na kwa kiwango cha kuridhisha.
IMEANDALIWA NA
KITENGO CHA MAWASILIANO NA UHUSIANO
MANISPAA YA KINONDONI.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.