Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mh Paul Makonda amezindua rasmi zoezi la ulipji wa fidia kwa awamu ya Kwanza kwa wakazi 179 wanaoathiriwa na mradi wa uboreshaji wa miundombinu (DMDP) kwa Manispaa ya Kinondoni.
Uzinduzi huo ambao pia umehudhuriwa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni Mh Benjamin Sitta umefanyika baada ya waathirika hao kukamilisha taratibu za kihasibu na kuwasilisha nyaraka zao na akaunti zao za kibenki baada ya Serikali kutoa idhini ya ulipwaji wa fidia katika Barabara za Makanya, Tandale-Kisiwani, Kilongawima na Simu 2000.
Amesema utekelezaji wa mradi huu unafanywa kwa awamu kulingana na mpango wa manunuzi(Procurement plan),uliokubaliwa kati ya Benki ya Dunia na Serikali kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI na Halmashauri.
Ameongeza kuwa katika mwaka wa Fedha 2016/2017 miradi iliyoanza kutekelezwa ni ujenzi wa barabara tano ambazo hazikuhitaji fidia kati ya Barbara kumi na moja zinazotakiwa kujengwa ambazo ni Makumbusho Sokoni, MMK, Nzasa, Tanesco, Soko la Samaki na barabara ya viwandani.
Akizitaja kazi zitakazofanyika katika mradi wa maendeleo na uboreshaji wa miundombinu, Makonda amesema kazi hizo zinahusisha maeneo muhimu kama ujenzi wa barabara zitakazopunguza msongamano katika Jiji la Dar Es Salaam, (Local roads), Uboreshji wa miundombinu katika makazi yasiyopangwa, na kuboresha mifereji ya maji ya mvua.
Ameongeza kuwa pia kutakuwa na mifumo ya kisasa ya ukusanyaji wa Mapato, kujenga uwezo katika miradi ya ubia kati ya Sekta binafsi na sekta ya Umma, na miradi unganishi kati ya miundombinu ya usafirishaji na matumizi ya ardhi.
Akizitaja barabara zilizoainishwa katika mradi huu wa uboreshaji wa Miundombinu Mthamini wa Manispaa hiyo ambaye pia hushughulikia maswala ya fidia Ndugu Reinhard Chidaga amesema Jumla ya barabara zilizoainishwa ni kumi na moja ambazo ni Makumbusho sokoni km 1.45, MMK km 0.9, Nzasa km 1.2,Tanesco -Msasani Soko la Samaki km 1.67, na Viwandani km 2.1.
Nyingine ni Makanya Km 5.10, Simu 2000 km 0.80, Kilimani Km 1.80, Tandale Kisiwani km 1.30, Maji Chumvi Kilungule Km 3.00 na Kilongawima km 1.80.
Mradi wa DMDP ulianza mwaka 2010 wakati huo ikiwa ni Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kabla ya mabadiliko ya kuanzishwa kwa Manispaa ya Ubungo .
Uboreshaji wa miundombinu katika maeneo yasiyopangwa unakusudia kuboresha makazi yanayokaliwa na wananchi wenye kipato duni na utahusisha Kata tatu za Tandale na Mwananyamala Manispaa ya Kinondoni, na Kata ya Mburahati Manispaa ya Ubungo.
Imetolewa na
Kitengo cha Uhusiano.
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.