Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mh. Paul Makonda ameonesha kuridhika kwake na hatua za ujenzi wa majengo ya utawala ya shule za msingi na sekondari, yanayoendelea kujengwa ikiwa ni awamu ya kwanza ya ujenzi wa takribani majengo 402, yanayotarajiwa kujengwa Mkoa wa Dar es salaam nje ya bajeti ya Serikali.
Hayo yamethibitika leo alipokuwa akikagua ujenzi wa jengo la utawala lenye ofisi nne,matundu ya vyoo pamoja na bafu, katika shule ya Sekondari Makumbusho ambapo ujenzi huo umekamilika.
Amesema dhamira yake ya dhati, pamoja na Serikali ya awamu ya tano chini ya Dr. John Pombe Magufuli ni kuona Mazingira ya waalimu wetu yanaboreshwa, hali itakayopelekea hari kubwa ya ufundishaji na kuleta matokeo chanya ya ufaulu kwa wanafunzi wetu.
Akionesha msisitizo wa azma yake hiyo nzuri amesema "lengo ni kujenga majengo ya utawala 402, ambapo 107 ni majengo ya utawala ya Sekondari, na 295 ni majengo ya utawala ya shule za Msingi, Kazi hii ya ujenzi haihitaji shukrani, bali shukrani ziende kwa Mungu, fanyeni kazi kwa faida ya Tanzania " amesema Makonda
Naye Katibu wa kamati ya ujenzi wa ofisi za waalimu Mkoa wa Dar es salaam, ambaye pia ni Afisa elimu wa Mkoa Mwalimu Khamis Lissu, amesema kwa sasa yanahitajika matofali milioni mbili, laki mbili na ishirini elfu, hadi majengo hayo kukamilika, na kuwataka wadau wa elimu kujitokeza kwa wingi kuchangia ili waweze kufanikisha azma hiyo.
Akitoa neno la shukrani, Afisa elimu Sekondari wa Manispaa hiyo, Ndg Rodgers Shemwelekwa amesema huo ndio uongozi unaoacha alama na ni mbegu inayoendelea kuchipua na isiyokufa katika sekta ya Elimu kwa kuthamini mchango unaotolewa kwa kutujengea majengo hayo ya utawala, na kuahidi kuyatunza kwa matumizi sahihi ili yalete tija kwa wanafunzi na Taifa la Tanzania kwa ujumla.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa wa Dar es salaam amewatakia watanzania wote mfungo mwema wa Mwezi mtukufu wa Ramadhan, na kuwaahidi usalama na utulivu katika kipindi chote cha Mfungo huo wa Ramadhan.
Imeandaliwa na
Kitengo cha Habari na Uhusiano.
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.