NI KUFUATIA UTEKELEZAJI WA AGIZO LA MKUU WA MKOA WA DAR ES SALAAM, MH PAUL MAKONDA, LA KUZITAKA KATA NA MITAA YOTE KUWA MISAFI.
Akifungua mkutano huo uliohusisha watendaji wa Kata, Mitaa pamoja na wadau wa maswala ya usafi, sheria na afya, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Dr. Patricia Henjewele amesema ni kwa lengo la kutathmini zoezi la usafi linaloendelea, na pia kukumbushana njia za kudhibiti na kutatua changamoto zinazojitokeza, wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo, ili ufumbuzi yakinifu wenye ufanisi uweze kuleta tija kwa maslahi mapana ya wananchi wa Kinondoni.
Amesema kukutanisha makundi haya muhimu pia kutawezesha kufikia malengo ya utekelezaji wa agizo hili ikiwa ni pamoja na kuhakikisha swala la changamoto linatatuliwa na kuweka mikakati thabiti itakayomwezesha kila mmoja kutimiza wajibu wake kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu katika kutekeleza agizo hili la Mkuu wa Mkoa, la kuhakikisha maeneo yote ya Kata na Mitaa yanakuwa safi.
"Tuna kama wiki mbili tangu tuanze zoezi hili la kuhakikisha jiji letu linakuwa safi, lakini ziko changamoto ambazo tumeona zimejitokeza, hivyo tumeamua kukutana ili kukumbushana jinsi ya kudhibiti changamoto hizi ili kazi yetu iweze kuwa na ufanisi mkubwa, na pia ni kutaka kukumbushana wajibu wetu katika hili, tusijejipangia majukumu ya ziada."Amebainisha Dr Patricia.
Akifafanua taratibu na wajibu wa mtumishi katika kutekeleza majukumu yake Bi Elly Makala Afisa kutoka Takukuru amesema wajibu wa Mtumishi ni kusimamia misingi ya sheria inayomtaka kutekeleza majukumu yake kwa uwazi, weledi na bila kumuonea mtu kutakakoondoa mianya ya rushwa.
Ameongeza kuwa Utumishi wa Umma hauna hiari bali wajibu katika kutekeleza limpasalo Mtumishi kwa wakati, hivyo kwa swala la usafi kila Mtumishi wa Umma akawe balozi wa usafi kwa kuwaelimisha wananchi umuhimu wake na adhabu atakayopatiwa mara baada ya kukiuka misingi ya usafi kwenye eneo Lake.
Akiainisha mada zitakazojadiliwa kwenye mkutano huo, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Dr. Patricia Henjewele amesema ufundishwaji wake ni kwa lengo la kuwasaidia kujua mipaka yao ya kazi ili kutoenenda kinyume na kusudio la sheria, na kuzitaja kuwa ni mada kuhusiana na sheria zinazohusiana na maswala ya rushwa, Ufafanuzi wa sheria zinazotakiwa kutumika wakati wa kusimamia maswala ya usafi, na wajibu umpasao mtendaji wa Kata au mtaa kusimamia wakati wa utekelezaji wa majukumu ya kiserikali.
Mkutano huo uliofanyika leo katika viwanja vya Manispaa, umehudhuriwa pia na wadau kutoka Takukuru, jeshi la polisi, vijana wa jeshi la mgambo, na vijana waliohitimu mafunzo ya JKT.
Imeandaliwa na
Kitengo cha Uhusiano na habari.
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.