Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni Ndugu Aron Kagurumjuli ametoa kauli hiyo leo alipokutana na wakandarasi hao kwenye ukumbi wa Manispaa kwa lengo la kuzungumza nao kufuatia kuwepo kwa malalamiko kutoka kwenye baadhi ya mitaa Kuwa kuna wakandarasi ambao hawafanyi majukumu yao kikamilifu hali inayopelekea uchafu kuzagaa kwenye baadhi ya maeneo.
Amesema wakandarasi hao wameomba zabuni ya kuzoa taka katika kata na mitaa jukumu lao la msingi ni hilo hivyo hakuna sababu yoyote kwao kuacha majukumu yao ya msingi kwa kigezo Cha kuwepo kwa utaratibu mpya wa ukusanyaji mapato kwani utaratibu huo hauathiri na Wala hautaathiri malipo yao kwa mujibu wa mkataba.
Akitoa ufafanuzi juu ya utaratibu mpya wa ukusanyaji wa mapato ya taka, Mkurugenzi Amesema kuwa wamefikia uamuzi wa kutumia utaratibu huo baada ya kufanya upembuzi yakinifu na kujiridhisha kuwa utaratibu huo utasaidia kudhibiti mapato ambayo hapo awali yalikuwa yakipotea.
Utaratibu wa sasa unamuacha mkandarasi na jukumu moja tuu la kuzoa taka na jukumu la kukusanya mapato linabaki kwa serikali ya mtaa, na mkandarasi atalipwa kwa mujibu wa kiwango Cha tripu (awamu) za taka alizozoa.
Aidha Mkurugenzi amewaagiza watendaji wa kata na mitaa kusimamia kikamilifu zoezi la uzoaji wa taka katika kata na mitaa yao huku akiwataka kutenga maeneo maalumu ambayo taka zitakusanywa hapo kwa siku maalum ili ziweze kufikiwa kwa urahisi na magari ya kuzolea taka.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni Mhe Benjamin Sitta amewasisitiza wakandarasi hao kushirikiana bega kwa bega na Halmashauri katika shughuli hizi za uzoaji taka kwani nia ya Halmashauri kuboresha namna ya ukusanyaji wa mapato ni njema kabisa na Halmashauri ipo tayari kupokea maboresho yoyote yatakayoonekana yanastahili.
Imeandaliwa na
Kitengo Cha Habari na Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.