Mkurugenzi Manispaa ya Kinondoni Ndg Aron Kagurumjuli kwa kushirikisha wadau wa elimu, ameahidi kushughulikia changamoto zinazoikabili sekta hiyo kwa upande wa Sekondari ili wanafunzi waweze kusoma katika mazingira mazuri na yenye kuridhisha yatakayochangia ufaulu katika masomo na mitihani yao.
Amebainisha hayo alipofanya ziara kutembelea na kukagua utekelezaji wa miradi mipya inayotekelezwa katika shule za Sekondari zilizopo kwenye Halmashauri yake.
Amesema atahakikisha changamoto hizo zinatatuliwa ili kuweka mazingira mazuri na salama kwa wanafunzi kusoma, na waalimu kufanya kazi kwa weledi.
Amezitaja changamoto hizo kwa kidato cha kwanza hadi cha nne kuwa ni upungufu wa matundu ya vyoo, huduma za umeme, upungufu wa maji,na uvamizi wa maeneo ya shule.
Nyingine ni masinki ya kufulia nguo, vifaa vya kupikia, ukamilishaji wa mabwalo na uzio wa shule kwa shule mpya za kidato cha tano na cha sita.
Aidha amemtaka Mhandisi pamoja na Afisa Elimu Sekondari wa Manispaa hiyo kufikia Julai mwaka huu, wafanye tathmini ya gharama zinazohitajika ili kukamilisha changamoto hizo ili shule hizo mpya ziweze kusajiliwa .
Miradi iliyotembelewa ni ujenzi wa shule ya Sekondari Mzimuni, mbezi juu, Mivumoni, kwa kidato cha kwanza hadi cha nne, na kwa kidato cha tano na sita ni Sekondari ya Tumaini girls na mbweni Teta .
Imeandaliwa na
Kitengo cha Habari na Uhusiano.
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.