Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mh. Daniel Geofrey Chongolo alipokutana na watendaji wa Kata na Mitaa, pamoja na wakuu wa idara na vitengo, katika kikao kazi kilichofanyika ukumbi wa Oysterbay shule ya Msingi leo.
Amesema kila, mtumishi wa Umma anao wajibu wa kutekeleza majukumu yake kwa wakati kwa kusimamia misingi ya sheria, kanuni na taratibu , ili kuepukana na migogoro inayoweza kuzuilika kwa mara moja.
"Sisi tukitimiza wajibu wetu, kwenye maeneo yetu, hakuna mtu atakayepeleka malalamiko Wilayani, Mkurugenzi weka utaratibu wa kila mtu kuwa part and parcel ya eneo lake la kazi" Amesisitiza Mh.Chongolo.
Kadhalika, amewataka watendaji wa Kata na Mitaa kuwa mstari wa mbele katika Kuzuia na kuepusha migogoro ya Ardhi, kuwa mstari wa mbele kukusanya mapato, kusimamia maswala ya usafi, na kujiepusha na viashiria vya rushwa.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni Ndg Aron Kagurumjuli, alipokuwa akitoa ufafanuzi wa mada za kikao kazi hicho, ameahidi kutekeleza maelekezo na maagizo yaliyotolewa na Mkuu huyo wa Wilaya, kwa kuwataka watendaji wa Kata na mitaa kuwa na takwimu sahihi za maeneo yao zikihusisha taarifa za wakazi, wafanyabiashara, masoko, maeneo ya uvuvi kwa waliopakana na bahari, wafugaji waliopo na aina ya mifugo wanayofuga, pamoja na takwimu sahihi za vibali vya ujenzi.
Pia amewataka watendaji hao kuhakikisha wanazingatia misingi na mkondo wa mawasiliano ulio sawia, wanajiepusha na migogoro ya kiutendaji, na kuzungukia maeneo yao ya kazi na si kukaa ofisini.
Aidha katika kikao kazi hicho, kilichoshirikisha wataalam kutoka sekta ya afya, biashara, mifugo, uchumi, Utumishi, kilimo, na elimu, kitaendesha mada sita ambazo ni wajibu na majukumu ya watendaji wa Kata, Usimamizi wa uendelezaji wa Miji, Usimamizi na uendelezaji wa daftari la mfanyabiashara, hatua sahihi za uanzishwaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo, pamoja na taratibu za manunuzi.
Hii ni mara ya kwanza kwa Mkuu huyo wa Wilaya kukutana na Watendaji wa Kata na Mitaa wa Manispaa ya Kinondoni tangu kuteuliwa kwake kuitumikia Wilaya hiyo.
Imeandaliwa na
Kitengo cha Uhusiano na Habari.
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.