Jumla ya Migogoro 17 ya ardhi imeripotiwa kushughulikiwa na kamati ya Mipangomiji na Mazingira, ndani ya kipindi cha robo ya tatu kuanzia mwezi wa kwanza hadi wa tatu Manispaa ya Kinondoni.
Hayo yamethibitishwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mh Songoro Mnyonge alipokuwa akiwasilisha taarifa yake ya utekelezaji robo ya tatu kwenye mkutano wa baraza la madiwani uliofanyika leo.
Amesema migogoro hiyo ya ardhi imehusisha uvamizi wa maeneo, mipaka ya viwanja, migogoro ihusuyo fidia pamoja na eneo moja kumilikiwa na mtu zaidi ya mmoja, hali iliyopelekea wananchi wenyewe kwa wenyewe kutoelewana.
Akiendelea kufafanua taarifa yake kwa Mstahiki Meya Manispaa hiyo Mh Benjamin Sitta, ambaye pia ni Mwenyekiti wa baraza la madiwani, Mh Songoro amesema kamati yake pia inalo jukumu kubwa la kuhakikisha inapanga mji na kusimamia upangaji huo kisheria, ikiwa ni pamoja na kutoa vibali mbalimbali vya ujenzi, baada ya kujiridhisha na uhalali wake.
Amesema katika kutekeleza hayo kamati yake imetoa vibali 32 vya kumiliki ardhi, 79 vya kuhamisha milki, 69 vya maombi ya upimaji ardhi, pamoja na leseni 72, za makazi kwenye maeneo yasiyopimwa.
Baraza hili la robo ya tatu pia limepitisha taarifa za utekelezaji za kamati ya fedha na uongozi, kamati ya nidhamu, kamati ya huduma za uchumi, afya na elimu,pamoja na kamati ya kudhibiti ukimwi na kutoa maazimio 12, yanayotakiwa kutekelezwa.
Imeandaliwa na
Kitengo cha Uhusiano na habari
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.