Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni Mhe. Songoro Mnyonge ameandaa ibada ya futari iliyohusisha wananchi wa Kinondoni, viongozi wa dini, viongozi wa vyama na Serikali pamoja na makundi mbalimbali hafla iliyofanyika katika viwanja vya ofisi hizo leo.
Akizungumza katika hafla hiyo Meya Songoro amesema lengo ni kujumuika pamoja katika mwezi mtukufu wa Ramadhan kama ishara ya kutenda wema, kufanya ibada na kuimarisha undugu katika kuienzi dhana ya toba na upendo kwa wananchi wake.
Amesema kujumuika pamoja kunaleta mshikamano uliodhahiri katika kutenda yale yanayompasa mwanadamu hasa dhana ya haki na kusisitiza umoja na mshikamano.
"Mwezi wa Ramadhan ni mwezi wa toba, matendo mema, ushirikiano na haki kwa waumini wa dini ya kiislam na katika kufanya hivyo mimi kama Mwenyekiti wa Halmashauri nimetamani kushirikiana na wananchi wangu ninaowajibika kwao katika ibada hii ya futari kama ishara ya ushirikiano, upendo na wema ili kwa pamoja tuweze kusimamia na kuenzi misingi ya haki katika uwajibikaji" Amesema Meya Songoro.
Katika hafla hiyo pia walishirikishwa Makao ya kulelea watoto yatima kutoka Malaika ambapo pamoja na shughuli nyingine walipatiwa vifaa mbalimbali ikiwemo vyakula kama ishara ya matendo mema kuelekea sikukuu ya Eid Al fitr.
Kadhalika alikuwepo pia Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Godwin Gondwe, Sheikh Mkuu Mufti Abubakar Zuberi Bin Ali, Sheikh wa Mkoa Ndg. Alhad Mussa Salum na Sheikh wa Wilaya ya Kinondoni Sheikh Mohamed Muyenga.
Waalikwa wengine ni Mwenyikiti wa BAKWATA Ndg. Ali Momba, Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu Taifa Sheikh Hamis Mattaka na Imam Mwenyekiti Mkuu wa BAKWATA Imam Mwita Kambi.
Kwa upande wao viongozi wa dini mbalimbali walipopata fursa ya kuzungumza, wamemshukuru Mstahiki Meya, pamoja na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo kwa kuandaa ibada ya futari iliyowakutanisha pamoja.
Imeandaliwa na
Kitengo Cha Habari na Uhusiano.
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.