Utengenezaji wa mbolea asilia (mboji) katika kiwanda kilichopo Kata ya Mabwepande kimesaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira ndani ya Manispaa ya Kinondoni.
Kiwanda hiki kilichopo Kata ya Mabwepande Manispaa ya Kinondoni kinajihusisha na ukusanyaji wa taka oza na kuzigeuza taka hizo kuwa mbolea asilia (mboji).
Akizungumza Meneja wa kiwanda hicho Jimson Mkenda akiwa ni mmoja wa washiriki wa maonesho ya Nane Nane katika banda la Manispaa ya Kinondoni amesema, dhumuni la kuanzisha kiwanda hicho ni kupunguza tatizo la hewa chafu katika mazingira yetu.
Amesema "kiwanda kimesaidia kuondoakana na hewa chafu, kimepunguza uchafuzi wa mazingira masokoni na katika makazi ya watu, kimetoa fursa ya ajira na kimesaidia taka oza kuwa malighafi ambayo ni mbolea asilia (mboji).
Vilevile, kiwanda kimesaidia jamii kuelewa umuhimu wa kutunza mazingira hasa kuelewa kuwa taka oza zinafaa kwa matumizi mengine. "Mwanzoni jamii haikuwa na uelewa juu ya matumizi ya taka oza baada ya kupata elimu taka hizo zinahifadhiwa kwa ajili ya kutengeneza mbolea ya asili (mboji)", Amesema Jimson.
Ameongeza kuwa, kutokana na uzalishaji mkubwa wa mbolea na elimu itolewayo kuhusiana na umuhimu wa mbolea hiyo masoko yameongezeka na kupelekea wakulima kupata mazao ya kutosha kwenye jamii na kupunguza tatizo la upungufu wa chakula". Amefafanua kuwa, kiwanda kinazalisha zaidi ya tani 50 kwa siku ambapo mpaka sasa zimeuzwa kilo 437,550 kwa wakulima wadogo na wakubwa.
Zubeda Mwaluka mkazi wa Morogoro ametembelea banda hili na kupata elimu juu ya mbolea ya mboji amesema, "mbolea hii inapunguza gharama ya mtu kutegemea ufugaji ndio apate mbolea". Ameongeza kuwa, kupitia mbolea hii itapunguza uchafuzi wa mazingira.
Kauli mbiu ya maonesho ya Nane Nane mwaka 2023 inasema, "Vijana na Wanawake ni Msingi Imara wa Mifumo Endelevu ya Chakula".
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini:
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.