Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa, ameuagiza uongozi wa Wilaya na Manispaa ya Kinondoni kuendelea kubuni namna nzuri ya kuhamasisha watu kushiriki mazoezi na yafanyike kila Jumamosi.
Alitoa agizo hilo wakati akizindua mbio za hiyari kwa ajili ya afya katika Fukwe za Coco Mei 4, 2024. Alisema, "Licha ya kuwa Kinondoni mna timu ya mpira wa miguu ya KMC, hakikisheni mnaandaa vilabu vya Jogging ili kushiriki michezo na mazoezi".
Aliongeza kuwa, "Kinondoni ina ukanda wa vivutio vya biashara hivyo eneo la fukwe za Coco litumike kwa ajili ya mazoezi kwa lengo la kuwakutanisha wana Dar es Salaam katika kufanya mazoezi hayo."
Nae, Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy Mwalimu, alisema kuwa lengo la kuanzishwa kwa mazoezi hayo ni kuwakinga wananchi wasipate magonjwa. "Mazoezi husaidia kukinga magonjwa ya sukari na shinikizo la juu la damu. Mazoezi ni afya na huleta furaha".
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Albert John Chalamila ameagiza mazoezi hiyo kuwa endelevu na kutoa wito kwa wana Dar es Salaam wote kukutana katika fukwe za Coco kila Jumamosi kwa ajili ya kufanya mazoezi hayo.
"Nawaagiza Katibu Tawala Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala Wilaya zote na Wakurugenzi wote wa Manispaa za Mkoa wa Dar es Salaam kuendelea kuratibu na kuhamasisha wananchi kushiriki Mbio hizo katika fukwe za Coco kila Jumamosi".
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.