Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni , leo imezindua Baraza la wazee ikiwa ni baada ya kufanyika kwa uchaguzi wa viongozi mwezi Juni mwaka huu.
Baraza hilo limezinduliwa na Katibu Tawala wa Halmashauri hiyo, Bi Stella Msofe , kwaniaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe Daniel Chongolo ambapo ameshauri baraza hilo litumike vema kwa wazee kushauriana namna ya matumizi sahihi ya kadi za msamaha za bima ya afya pamoja na kupaza sauti juu ya changamoto wanazokumbana nazo.
Bi Msofe ameongeza kuwa wazee ni hazina inayotakiwa kutunzwa ipasavyo kwakuwa ni chachu ya maendeleo ya nchi jambo ambalo hata serikali ya awamu ya tano imekuwa mstari wa mbele kujali afya zao.
Amefafanua kuwa serikali ya awamu ya tano, inawajali wazee na makundi yote ya kila rika, na kwamba kuna haja ya kutoa elimu kuhusu matumizi ya kadi ya afya kwa wazee na hivyo kutoa jukumu hilo kwa wajumbe wa baraza hilo.
Viongozi wa baraza hilo waliochaguliwa Juni mwaka huu ni Wallace Mwakikalo kutoka Kata ya Kigogo ambaye ni mwenyekiti, Hapendeki Mshambya Makamu mwenyekiti kutoka Kata ya Kunduchi, Richard Kisika Katibu kutoka Kata ya Mbezi juu.
Wengine ni Maua Mtiga ambaye ni Katibu msaidizi kutoka Kata ya Makumbusho, Jaha Kimvuli mtunza hazina kutoka Kata ya Ndugumbi, Mary Kallinga mjumbe kutoka Kata ya Mzimuni na Khalid Mntambo mjumbe kutoka Kata ya Magomeni.
Katika hatua nyingine Bi Msofe ameipongeza idara ya afya kwa kazi kubwa walioifanya ya kuendesha zoezi la utoaji chanjo ya surua pamoja na Polio na kusema kuwa huduma hiyo imewafikia wananchi kwa asilimia kubwa.
Imetolewa na
kitengo cha Habari na Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.