Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni Ndg Aron Kagurumjuli amesaini mikataba miwili ya ujenzi wa barabara chini ya mradi wa uboreshaji wa Jiji la Dar Es Salaam (DMDP) zenye thamani ya zaidi ya bilioni hamsini
Mikataba hiyo imesainiwa leo katika ukumbi wa mikutano wa Manispaa uliopo Magomeni, na kuhudhuriwa na Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo, wataalam wa ujenzi kutoka Manispaa, na wakandarasi waliopewa jukumu la ujenzi.
Akizitaja barabara hizo kuwa ni barabara ya Makanya, tandale kisiwani, kisukulu, korogwe, external na kilungule ambazo zipo kwenye awamu ya Pili na ya tatu ya mradi, Mkurugenzi huyo wa Manispaa amesema zitajengwa kwa kiwango cha lami nzito kitakachokidhi matakwa na mahitaji kwa ubora uliokusudiwa.
Aidha amebainisha kampuni zitakazohusika na ujenzi wa barabara hizo kuwa ni kampuni ya China civil Engineering Construction Operation, kutoka nchini China, na kampuni ya hapa nyumbani ya Estim Construction Company. Ltd ambazo mbali na ujenzi wa kiwango cha lami, pia zitajenga sehemu ya wapita kwa miguu, mifereji ya maji ya Mvua, Madaraja, Calvart pamoja na uwekaji wa taa na alama za barabarani.
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Mh. Benjamin Sitta amempongeza Mkurugenzi kwa kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha barabara za awamu ya kwanza ya mradi, zimejengwa kwa ubora uliokusidiwa.
Aidha amewataka wananchi watumiaji wa barabara hizo kuwa wazalendo kwa kuhakikisha wanazitunza, wanazipenda, na kuzilinda ili ziweze kudumu kwa muda mrefu zaidi na ziweze kutumika kwa vizazi vijavyo.
Ujenzi wa barabara hizo unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi kumi na tano kuanzia octoba 2,mwaka 2017.
Imetolewa na
Kitengo Cha Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.