Semina ya mafunzo maalum kwa walimu wakuu wa shule za msingi za serikali na binafsi inayolenga kutoa mafunzo yanayohusiana na utekelezaji wa mtaala mpya wa elimu imefunguliwa rasmi katika Wilaya ya Kinondoni Mei 30 2024 katika ukumbi wa Soko la Magomeni. Mafunzo haya yamepangwa kwa lengo la kuwajengea uwezo walimu wakuu ili waweze kuelewa na kutekeleza mabadiliko ya mtaala kwa ufanisi katika shule zao.
Akizungumza katika Ufunguzi wa Semina hiyo Mthibiti Mkuu Ubora wa Shule Manispaa ya Kinondoni ambaye ndiye Mgeni Rasmi katika semina hiyo Bi.Naitwa Solomon Mghumba alitoa shukrani kwa Serikali kutoa mafunzo hayo kwa walimu wakuu na kuahidi kuunga mkono mafunzo hayo kwa kuanzisha na kuendeleza mafunzo ya ziada ya ziada kwa walimu ili waweze kuelewa na kuendana na mtaala mpya wa elimu.
"Tunashukuru na kuipongeza serikali kwa kutoa mafunzo haya.Kinonfoni tumeyapokea vizuri mafunzo haya na sisi tutaendelea kuandaa mafunzo yetu ya ndani ili kuwajengea walimu uwezo utakaowasaidia kuwafundisha wanafunzi vizuri na wataalam bora wa baadaye."
Washiriki wa mafunzo haya ikiwemo Waratibu wa Mafunzo ngazi ya Mkoa na Wilaya, Wawezeshaji na Walimu Wakuu walipata fursa ya kujadili na kuelewa vipengele mbalimbali vya mtaala mpya, ikiwa ni pamoja na mbinu za ufundishaji, tathmini za wanafunzi, na matumizi ya teknolojia katika kufundishia. Aidha, walimu wakuu walihimizwa kuwa viongozi na mfano bora katika shule zao, wakihakikisha kuwa mtaala mpya unatekelezwa kikamilifu.
Mafunzo haya yatakayofanyika kwa siku mbili kuanzia Mei 30 2024 mpaka Mei 31 2024 yanatarajiwa kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya Elimu ya Msingi katika Wilaya ya Kinondoni, huku yakitoa mwongozo muhimu kwa walimu wakuu katika kuboresha ufundishaji na ujifunzaji. Serikali na wadau wa elimu wameeleza kuwa wataendelea kutoa msaada na rasilimali zinazohitajika ili kuhakikisha kuwa mtaala mpya unafanikiwa.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.