Manispaa ya Kinondoni imeandaa mafunzo kazi ya siku moja kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Kata yenye lengo la kuwajengea uwezo katika matumizi ya mfumo wa utoaji na usimamizi wa fedha zitokanazo na asilimia kumi ya mapato ya ndani ya Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Akifungua mafunzo kazi ya mfumo wa utoaji na usimamizi wa mikopo leo tarehe 18 Juni, 2022 katika ukumbi wa mikutano wa Manispaa ya Kinondoni, Kaimu Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Bw. John Deogratius amesema matumizi ya mfumo huo wa kielektroniki ni suluhisho ya changamoto mbalimbali za utoaji na usimamizi wa fedha za umma ikiwemo uwepo wa vikundi hewa na utoaji wa mikopo kwa wasiolengwa.
"Mfumo unawezesha utambuzi wa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa ufanisi, uwazi na udhibiti wa mianya ya upotevu wa fedha za Serikali pamoja na kuwezesha upatikanaji wa taarifa mbalimbali kwa usahihi na kwa wakati. Niwaombe sote tushiriki mafunzo kazi haya kwa ufanisi ili tuweze kwenda kusimamia utoaji wa mikopo pamoja na marejesho yake kwa weledi". Amefafanua, John Deogratius.
Mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri imekuwa ikitolewa katika Halmashauri zote nchini kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu ili kuwawezesha kuanzisha na kuendeleza shughuli zao za ujasiriamali zitakazowawezesha kujiongezea kipato na kushiriki kikamilifu katika ukuaji wa uchumi.
Mafunzo kazi hayo yamehusisha Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Kata zote 20 za Manispaa ya Kinondoni ikiwa ni maandalizi ya matumizi ya mfumo mpya wa kielektroniki unaotarajiwa kuanza rasmi kutumika kuanzia tarehe mosi Julai, 2022.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.