Mafunzo hayo yaliyoendeshwa na shirika lisilo la kiserikali la Save the children, kwa kushirikiana na PDF yaliyolenga kutoa upeo na kuainisha umuhimu wa watoa maamuzi, kushiriki katika uaandaaji na upitishaji wa bajeti yenye vipaumbele vya mtoto, yamefanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa Manispaa.
Akifafanua mafunzo hayo mratibu wa usalama wa mtoto kutoka shirika la Save the Children, Bi.Haika Harrison amesema, mafunzo haya yamelenga mpango madhubuti wa maandalizi ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2019/2020, iliyorafiki kwa mtoto, inayozingatia huduma muhimu zihusuzo haki ya kuishi na kuendelezwa, elimu, afya, ulinzi pamoja na usalama.
Aidha ameeleza pia umuhimu wa kuandaa bajeti kwa kuzingatia vipaumbele vya watoto na kuvitaja kuwa ni kurahisisha utekelezaji wa mipango inayowahusu watoto, kuratibu shughuli mbalimbali, ni nyenzo ya mawasiliano pamoja na kuwa sehemu ya udhibiti wa rasilimali.
Naye Bi Neema Bwaira ambaye ni mtaalam wa haki za watoto na utawala bora kutoka shirika la Save the children alipokuwa akitoa mada kuhusiana na uandaaji wa bajeti iliyorafiki kwa mtoto amesema, zipo kanuni za kuzingatia wakati wa uandaaji bajeti iliyorafiki kwa mtoto ambazo ni kutobaguliwa kwa mtoto, kuweka mbele maslahi ya mtoto na umuhimu wa mtoto kujieleza na kutoa maoni.
Ameainisha pia sifa ya bajeti ambayo ni rafiki kwa mtoto kuwa ni ile inayotekeleza sera za kiuchumi na za jamii ambazo ni rafiki na zinamaslahi mapana kwa watoto, inayoangalia mahitaji yao muhimu hasa waishio katika mazingira magumu.
Nyingine ni ile inayogusa sekta muhimu kama vile elimu, afya, maji safi, usafi wa mazingira, ni ile inayotoa fursa sawa za maendeleo na kuheshimu haki za watoto bila kujali makabila, dini, mikoa au rangi, na yenye kutengeneza mfumo bora na wezeshi katika mtiririko wa rasilimali unaomfikia mtoto kwa wakati.
Akichangia mada hiyo ya uaandaaji wa bajeti, Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye pia ni Naibu Meya wa Manispaa Mh.Manyama Mangalu amesema, swala hili ni la kisera zaidi, na ni vema ikatolewa elimu ya kutosha juu yake, ili upatikane ufumbuzi wa kudumu unaomjali na kumthamini mtoto.
Mafunzo haya yamepata uwakilishi kutoka WAMATA, Right to Play, SISEMA na waku wa Idara na vitengo.
Imeandaliwa na
Kitengo cha Uhusiano na Habari.
Manispaa ya kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.