Madawati ya jinsia katika masoko yametakiwa kutunza siri za wateja wanaowahudumia.
Hayo yalibainishwa Disemba 20, 2023 na Bi. Reinfrida Mathayo, ambaye ni Kiongozi wa Ujumbe kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum. Bi. Reinfrida aliongoza ujumbe huo uliotembelea Manispaa ya Kinondoni kwa lengo la kukagua utendaji wa madawati hayo maeneo ya Masoko.
Alisema kuwa, "ujio wetu ni kuleta ujumbe Maalum kutoka kwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia na Makundi Maalum Dkt Doroth Gwajima, unaoyataka Madawati haya kulinda siri kwenye mashauri wanayoyasikiliza. Hii itasaidia kuondokana na unyanyapaa na ubaguzi unaoweza kutokea wakati wa kuyashughulikia malalamiko ya wateja wenu."
Aliongeza kuwa, Wizara inataka kuona huduma zinazotolewa na Madawati hayo zinakidhi matakwa ya Jamii ikiwemo utunzaji wa siri.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Kinondoni, Bw. Alex Ntiboneka, alisema kuwa, "ujio wa ujumbe huo ni ishara ya ufuatiliaji wa kuona namna wanavyotekeleza maagizo wanayopatiwa na Wizara." Aidha Bw. Ntiboneka aliahidi kufanyia kazi maelekezo yote ya Wizara kwa weledi.
Ukaguzi wa Madawati hayo ulifanyika katika masoko ya Kata za Makumbusho, Tandale, Mzimuni na Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.