DC HAPI KWA NIABA YA MKUU WA MKOA WA DAR ES SALAAM AWA MGENI RASMI.-ASISITIZA UMUHIMU WA UPANDAJI NA UTUNZAJI WA MITI.
Maadhimisho ya wiki ya upandaji miti ngazi ya Mkoa, yameadhimishwa katika Manispaa ya Kinondoni kwa kupanda takriban miti 800 kwenye maeneo mbalimbali ya Mkoa huo ,kutoka katika vitalu vya wakala wa misitu (TFS) kwa kushirikiana na Halmashauri za Mkoa wa Dar es salaam.
Akiongea katika maadhimisho hayo, yaliyofanyika katika Kata ya Kunduchi, Manispaa ya Kinondoni, Mkuu wa Wilaya hiyo, Mh. Alli Hapi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam amesema siku hii ni muhimu Sana kwa wananchi kushiriki ili kwa pamoja tuweze kufikisha ujumbe mahususi kwa jamii kuhusiana na umuhimu wa upandaji miti, utunzaji na usimamizi wake.
"lengo ni kutumia siku hii maalum kufikisha ujumbe kwa jamii yetu, juu ya kuihamasisha Jamii katika swala zima la upandaji miti, utunzaji na usimamizi wake, na matumizi endelevu juu ya rasilimali zetu za misitu. "Amesema Hapi
Akifafanua kuhusiana na kauli mbiu ya mwaka huu isemayo "Tanzania ya Kijani inawezekana panda miti kwa Maendeleo ya viwanda" amesema ni muhimu Sana Tanzania yetu ya viwanda ikaendana na zoezi la upandaji miti kwani kwa kufanya hivyo itapunguza uharibifu wa tabaka la juu la anga(ozone) itokanayo na uzalishwaji wa hewa ya ukaa, ambapo uharibifu unapotokea husababisha miale ya moja kwa moja kushuka na kuumiza viumbe hai.
Ameongeza kuwa upandaji wa miti na utunzaji wa Mazingira ni ajira nzuri kwa vijana, kwani Mazingira yawapo mazuri na safi huwa vivutio kwa watu kupumnzika na kufanya shughuli zao .
Aidha amezitaka Halmashauri zote za Mkoa wa Dar es salaam kuweka mifumo ya maji katika barabara zilizopandwa miti ili kuweza kurahisisha umwagiliaji.
Awali akitoa taarifa mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, mwakilishi wa wakala wa huduma za misitu nchini (TFS) Bi Dyaga Follen Mkomwa, amesema siku hii ya upandaji miti kitaifa inatokana na waraka wa Serikali namba moja wa mwaka 2000 ,ambapo kila Wilaya nchini inatakiwa kupanda miche ya miti milioni moja na laki tano kila mwaka.
Ameongeza kuwa misitu iliyopo katika Mkoa wa Dar es salaam pamoja na upandaji huu wa miti ni jitihada za viongozi mbalimbali wa Serikali katika kusimamia utunzaji Mazingira, ambayo inasaidia kuboresha Mazingira na kufyonza hewa ukaa inayozalishwa viwandani kwa sasa, na pia kukabiliana na ongezeko kubwa la hewa ukaa itakayozalishwa kutokana na mkakati uliopo wa kuongeza viwanda katika Mkoa wa Dar es salaam.
Maadhimisho haya kimkoa yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa vyama na serikali kutoka katika Halmashauri zote za Mkoa wa Dar es salaam, ambapo Kitaifa yanadhimishwa mkoani Shinyanga katika wilaya ya Kishapu.
Imeandaliwa na
Kitengo Cha habari na uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.