Akizingumza katika maadhimisho hayo yanayoenda kwa kauli mbiu ya Kitaifa isemayo "zingatia usawa, tokomeza UKIMWI,tokomeza magonjwa ya mlipuko" mgeni rasmi ambaye pia ni Naibu Meya wa Manispaa hiyo Mheshimiwa Kheri Misinga ameishukuru Serikali kwa kuweka hatua hii ya maadhimisho Kiwilaya kwani ni fursa pekee na ndio msingi imara wa kutathmini hali ilivyo sasa, tulikotoka na tunakokwenda hasa ikizingatiwa elimu katika suala hili la VVU na UKIMWI ni muhimu sana.
Amesema kuwa kufanyika maadhimisho haya pia ni kuimarika kwa demokrasia katika Halmashauri hali inayoleta ushirikiano katika kuhakikisha jamii inafikiwa kwa huduma zote muhimu ikiwemo elimu, afya na huduma za upimaji na chanjo.
Alipokuwa akitoa ufafanuzi wa hali ya upimaji na asilimia za maambukizi, Mganga Mkuu wa Manispaa hiyo Dkt. Samweli Laizer amesema hali imeendelea kuimarika na uelewa wa maambukizi ya VVU na UKIMWI kwa sasa ni mkubwa sana na kuwataka wananchi kutopuuza na kuhakikisha wanapima afya zao kabla ya kujihusisha na ngono zembe au kuingia katika mahusiano
Naye mratibu wa UKIMWI Manispaa ya Kinondoni Bi. Rhoby Gweso alipozungumza amesema lengo la kufanya maadhimisho eneo la Tandale uwanja wa sifa ni kufikisha elimu sahihi kwa wahusika na jamii kwa ujumla kuhusiana na madhara ya UKIMWI, ikiwa ni pamoja na kuwasisitiza umuhimu wa kutojihusisha na ngono zembe, pamoja na biashara ya kuuza miili yao.
Alipokuwa akisoma taarifa kwa niaba ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI Kinondoni (WAVIU) ndugu Isakwisa Jeremiah amesema wanaishukuru Manispaa hiyo kwa kuwa mstari wa mbele kushirikiana nao hasa pale wanapohitaji msaada wa karibu ikiwa ni pamoja na kuiomba Serikali kuhakikisha Afua za VVU na lishe zinaelekezwa kwa kundi maalumu la vijana kwani ndio walengwa wakubwa.
Maadhimisho hayo yaliyofanyikia katika Kata ya Tandale viwanja vya sifa yamehusisha wadau mbalimbali kama "Steps Tanzania", Care for AIDS, TAYOBECO, TAWIDO, YOP, PHSRF na MDH, ambapo shughuli mbalimbali zilifanyika ikiwemo kukabidhi misaada kwa WAVIU 52, upimaji wa VVU na chanjo ya UVIKO-19.
Kadhalika maadhimisho hayo pia yaliyohudhuriwa na wajumbe wa Kamati ya kudhibiti UKIMWI, Wakuu wa Idara na Vitengo pamoja na wadau wengine waliwasha mishumaa kama ishara ya kuwakumbuka wapendwa wao waliotangulia mbele za haki, lakini pia yalipambwa na burudani kutoka kwa msanii Salum Jabiri (Msaga Sumu), Bambo pamoja na Mtanga.
Imeandaliwa na
Kitengo cha Habari na Uhusiano.
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.