Ni kauli yake Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan, alipokuwa akihutubia katika kilele cha maadhimisho ya Mazingira yaliyofanyika Kitaifa katika viwanja vya mnazi mmoja Jijini Dar es Salaam.
Amesema katika kilele cha maadhimisho haya chenye kauli mbiu isemayo "Mkaa ni gharama, tumia nishati mmbadala", tunao wajibu wa kukumbushana na kuelimishana athari zitokanazo na ukataji wa miti kiholela.
Amezitaja athari hizo kuwa ni kukimbiza wanyama, kupoteza Matunda asilia, kuharibu makazi ya wadudu wenye kazi mbalimbali, kuharibu misitu inayotusaidia kunyonya joto au hewa ukaa na bahari kuingia eneo la mkazi ya watu.
Aidha Mh Samia Suluhu, ameainisha pia changamoto zitokanazo na uharibifu wa mazingira kuwa ni kuharibika kwa vyanzo vya maji, pamoja na mfumo wa ikolojia na kuwataka wananchi kuwa mstari wa mbele kulinda na kuheshimu mazingira ikienda sambamba na mikakati ya matumizi sahihi ya ardhi, pamoja na juhudi madhubuti zinazozingatia umuhimu huo zikilenga ukuaji wa uchumi wa viwanda.
Naye Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Mazingira Mh Januari Makamba alipokuwa akimkaribisha Makamu wa Rais amesema siku ya kilele cha Mazingira ni siku ya kutathimi na kujiridhisha uwepo wa Uhusiano mkubwa kati ya Maendeleo na Mazingira,uliofungamana na ustawi wa wananchi wetu.
Akitoa salaam za mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa mkoa huo Mh Paul Makonda amezitaja changamoto zilizo katika mkoa wake kuwa ni swala la mafuriko linalopelekea nyumba kubomoka na wananchi kupoteza maisha, pamoja na uchafu wa Mazingira unaosababishwa na wananchi wenyewe na kutangaza tarehe 01/07/2018 kuwa siku ya usafi mkoa wa Dar es salaam.
Aidha maadhimisho hayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa vyama na serikali na kuburudishwa na vikundi vya ngoma, brass band pamoja na wimbo wa Mazingira kutoka kwa msanii wa kizazi kipya Beka flavour.
Imeandaliwa na
Kitengo cha Uhusiano na Habari
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.