Kuelekea siku ya kilele cha Mtoto wa Afrika chenye kauli mbiu isemayo "Mtoto ni msingi wa Taifa endelevu tumutunze, tumlinde na kumuendeleza", Kinondoni yaadhimisha kwa kutoa zawadi mbalimbali kwa watoto wenye uhitaji maalumu pamoja na michezo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni katika sherehe hizo zilizofanyika Kiwilaya katika shule ya msingi Magomeni, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Bi. Stella Msofe amesema watoto ni hazina ya Taifa, hivyo wanapaswa kulindwa, kutunzwa, kuthaminiwa, kuheshimiwa na kubwa zaidi kuwapatia haki za msingi kama elimu na afya.
Ameongeza kuwa wakati umefika wa Serikali kutofumbia macho unyanyapaa wa watoto wenye mahitaji maalumu hususani ulemavu wa viungo vya mwili kwani wanayo haki na nafasi sawa katika jamii, hivyo wapewe nafasi wanayostahili na kupatiwa vipaumbele kama watoto kwani ndio warithi wa baadae wa Taifa hili.
"Leo hii Tanzania tunajivunia maendeleo yanayosimamiwa na Mh Rais Dr. John Pombe Joseph Magufuli, naye aliwahi kuwa mtoto akakuwa, akatunzwa akapewa haki zake, na leo hii ndiye kiongozi shupavu, yote hii ni kwasabababu aliandaliwa vema mpaka amekuwa na uwezo huo na sisi kama jamii tukitenda haki sawa kwa kuwathamini wote bila kujali hali zao, tutakuwa tunaandaa viongozi bora wa baadae" amesisitiza Bi Stella.
Naye Bi. Halima Kahema ambaye ni Mkuu wa Idara ya idara ya maendeleo ya jamii katika Manispaa hiyo akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi amesema Manispaa yake iko tayari kushirikiana na Asas hizi katika kuhakikisha haki ya mtoto inatekelezwa na wahitaji wananufaika nayo.
Katika maadhimisho hayo yaliyoambatana na utoaji wa vyeti vya ushiriki za Asas sita, pamoja na zawadi za madaftari na fulana kwa watoto, pia yalipambwa na michezo ya kukimbia, kuruka kamba na kukimbiza kuku .
Asas zilizoshiriki katika maadhimisho hayo ni Kihowede, AHRN, Save the children, PDF (peopale development forum), Red cross na Tiba.
Imeandaliwa na
Kitengo Cha Habari na Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.