Manispaa ya Kinondoni kwa kushirikiana na Asasi ya vijana ya YOP kuelekea kilele cha siku ya Ukimwi duniani, imehamasisha vijana kupima na kujua afya zao ili waweze kujilinda na kujiepusha na maambukizi dhidi ya VVU.
Hayo yamethibitika leo katika tamasha la michezo lililoshirikisha vijana na wadau mbalimbali wanaoshiriki mapambano ya kudhibiti ukimwi ikiwa ni hatua ya maandalizi kuelekea kilele cha maadhimisho hayo ya UKIMWI kwa kuwataka vijana kupima afya zao.
Akiongea katika maadhimisho hayo kwa niaba ya mgeni rasmi, Mtendaji wa kata ya Mwananyamala Ndg. Mikidadi S. Ngatupura amesema, afya ndio msingi wa maendeleo, hivyo kwa vijana kujua hali zao mapema itawapa fursa ya kujiwekea malengo yao katika kusukuma gurudumu la maendeleo
"Vijana lazima mtambue afya zenu ili muweze kuyaishi malengo yenu, kama si afya bora hamuwezi kufikia malengo mliojiwekea, nawasihi mjiepushe na mambo yote ambayo yanaweza kupelekea kupata maambukizi ya virusi vya UKIMWI."Amesisitiza Mtendaji.
Kwa upande wake mwakilishi wa shirika la JHPIEGO Bi Happy Temu akitoa matokeo ya vipimo vya afya vilivyofanyika uwanjani hapo amesema uelewa umekuwa mkubwa kwani kati ya vijana 102, waliojitokeza kupima ambapo wasichana ni 33, na wavulana ni 69, matokeo yanaonesha kutopatikana kwa yeyote mwenye maambukizi ya virusi vya UKIMWI.
Katika hatua nyingine, maadhimisho hayo yalienda sambamba na mashindano ya mpira wa miguu ambapo timu za Mwenge combaini FC na African People zilichuana vikali na Mwenge combaini kuibuka kidedea kwa kumbamiza African people bao 2 kwa 1.
Maadhimisho haya pia yalipata ushiriki kutoka shirika la UNA, WAMATA pamoja na baraza la watu wanaoishi na virus vya UKIMWI.
Imeandaliwa na
kitengo Cha Habari na Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.