Wajumbe wa Kamati ya siasa kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kinondoni wamepongeza Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Manispaa ya Kinondoni kwa kuweza kufikisha ujumbe kwa jamii kupitia mitandao ya kijamii.
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Kinondoni Mhe. Shaweji Mkumbula wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa ndani ya Manispaa ya Kinondoni.
"Nichukie nafasi hii kukipongeza Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kwa kuanzisha KMC Online Media itakayosaidia jamii kupata taarifa na kuwapa fursa wananchi kutoa maoni yanayohamasisha kuleta maendeleo ya Wilaya ya Kinondoni". Amesema Mhe. Mkumbula.
Aidha Mhe. Mkumbula amesema kuwa wananchi washirikishwe kwenye kila mradi kwa kupewa taarifa kuhusiana na kila kinachoendelea katika Wilaya ya Kinondoni. "Taarifa zitolewe kwenye tovuti ya Manispaa ya Kinondoni kwa kushirikiana na tovuti ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kinondoni ili jamii iwe na uelewa kuhusu maendeleo ya nchi."
Katika ziara hiyo Mhe. Shaweji aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Saad Mtambule, Katibu Tawala Wilaya ya Kinondoni Bi. Stella Msofe, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni Mhe. Songoro Mnyonge, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni Bi. Hanifa Suleiman Hamza na Wakuu wa Idara katika Manispaa ya Kinondoni.
Miongoni mwa miradi iliyotembelewa ni pamoja na mradi wa ujenzi wa Soko la Tandale, mradi wa ujenzi wa jengo la mionzi, mradi wa ujenzi wa shule ya Msisiri B, na mradi wa madarasa ya BOOST shule ya msingi Mchangani.
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini:
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.