Akizindua zoezi hilo katika soko la Mwenge, Mkuu wa Wilaya ya Kinondonii Mh. Daniel Chongolo amesema, ni katika kutekeleza agizo la Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dr. John Pombe Joseph Magufuli, la kuwajengea mazingira mazuri wafanyabiashara wadogowadogo kwa kuwatambua na kuwapatia vitambulisho watakavyovitumia katika kazi zao.
Amesema ni zoezi endelevu, kwani vitambulisho hivi vilivyotengenezwa na Ofisi ya Rais -TAMISEMI vimelenga wafanyabiashara wenye mtaji chini ya milioni nne na pia ni kwa lengo la kuwawezesha mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwa na idadi na takwimu sahihi itakayowawezesha kwa urahisi kufanya kazi yao ya kukusanya mapato.
"Tumefanyia zoezi hili hapa Mwenge, kwani ndiko kuliko na wafanyabiashara wengi na vitambulisho hivi vimetolewa kwa lengo la kuwezesha mamlaka ya mapato Tanzania kutambua wafanyabiashara wadogowadogo, pia litawasaidia wafanyabiashara wetu kufanya biashara bila bugudha yeyote." Amesisitiza Mkuu huyo wa Wilaya.
Naye Afisa Biashara wa Manispaa hiyo Bw. Mohamed Nyasama alipotakiwa kuzungumzia swala hilo amesema, hii ni neema kwa wamachinga kwani kitakachofanyika ni kuwatambua, kuwahakiki, na kuwapatia vitambulisho hivyo vitakavyowasaidia kufanya biashara sehemu yoyote nchini bila usumbufu wowote.
Amesema kinachotakiwa kufanyika ni kwa wafanyabiashara waliokwisha hakikiwa kujaza fomu za usajili, kuwasilisha picha, na vitambulisho ambavyo walikwishapatiwa na Manispaa awali, ili waweze kupatiwa vipya na kwa wale wamachinga ambao hawana vitambulisho kuhakikiwa upya na kupatiwa vitambulisho kwa mujibu wa sheria.
Aidha zoezi hili pia limehusisha wamachinga kutoka masoko ya Bunju A, na B, Morocco, Boko Basihaya, Mbezi samaki, Mbezi ya Chni,Tegeta, Kawe, Mwenge, Makumbusho, Magomeni, Mwananyamala na Tandale.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Wilaya amewataka wamachinga hao kuhakikisha wanazingatia sheria, kanuni, na taratibu katika matumizi ya vitambulisho hivyo, ili kuepukana na usumbufu wowote unaoweza kutokea na kuhakikisha kila muhusika ananufaika na zoezi hili.
Imeandaliwa na
Kitengo cha habari na Uhusiano.
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.