Manispaa ya Kinondoni, leo imezindua rasmi maadhimisho ya sherehe za miaka 61 ya Uhuru.
Uzinduzi huo umefanyika katika shule ya Sinza Maalum iliyopo Kata ya Kijitonyama kwa kushiriki shughuli za usafi na upandaji miti shuleni hapo.
Akizungumza na baadhi ya wananchi waliojitokeza katika uzinduzi huo, mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa ambaye pia ni Mchumi wa Manispaa, Bw. Jabir Chilumba, amesema maadhimisho ya sherehe za Uhuru kwa Manispaa ya Kinondoni yaliyoanza leo yataadhimishwa kwa kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii. Alisema, "Kinondoni tumezindua leo, tutafanya shughuli za kijamii za usafi, upandaji miti katika maeneo mbalimbali ya taasisi za Elimu, Afya nk. Aidha tutafanya mashindano ya uandishi wa insha kwa wanafunzi wa shule za msingi na tutahitimisha kwa kufanya mdahalo".
Bw. Chilumba alisema, "Mdahalo huo utazungumzia mafanikio ya kiuchumi na kijamii yaliyopatikana ndani ya miaka 61 ya Uhuru wa nchi yetu. Hivyo wananchi tunawakaribisha kushiriki mdahalo huo."
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na Diwani wa Kata ya Kijitonyama, Mheshimiwa Damas Samira Lusangija, aliwaongoza wananchi waliohudhuria uzinduzi huo kupanda miti ya kivuli na matunda.
Mheshimiwa Lusangija alisema, tunashukuru kwa kuichagua Kata ya Kijitonyama kuzindua maadhimisho haya kiwilaya. Nawaomba wananchi kuendelea kufanya shughuli mbalimbali zilizopangwa ndani ya Wiki hii ya Uhuru."
Maeneo mengine yatakayofanyiwa usafi ni ya fukwe zilizopo ndani ya Manispaa ya Kinondoni. Aidha mashindano ya vikundi vya sanaa yatafanyika Makumbusho. Kilele cha maadhimisho haya kitafanyikia Disemba 9 kwa kufanya mdahalo katika ukumbi wa Manispaa ya Kinondoni.
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini: Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.