Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imewawezesha wananchi kiuchumi kwa kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi za Kitanzania bilioni 3.9 katika mwaka robo ya nne ya mwaka (Aprili-Juni) wa fedha 2021/2022 kupitia asilimia kumi ya mapato yake ya ndani kwa jumla ya vikundi 286, ambapo kati yake vikundi 182 vikiwa ni vya wanawake, vikundi 90 vya vijana na vikundi 14 vya watu wenye ulemavu.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya hundi ya mfano mgeni rasmi Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Godwin Gondwe ameipongeza Halmashauri kwa jinsi ambavyo imeweza kufanya usimamizi na utoaji wa mikopo kwa makundi hayo maalum na kuhakikisha kwamba maagizo ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kuhusu utoaji mikopo bila riba yanatekelezwa na kuwafikia walengwa kwa wakati.
“Niwapongeze wanufaika wote wa mikopo ya asilimia kumi na ambao mnafanya marejesho kwa wakati”. Unaporejesha mikopo unatoa fursa kwa vikundi vingine vyenye sifa kuweza kukopa lakini pia unajijengea sifa ya kukopeshwa kwa mara nyingine. Alifafanua Gondwe.
Mkuu wa Wilaya pia ametoa ahadi ya kushirikisha taasisi mbalimbali za Serikali na binafsi ikiwemo SIDO, BRELA na taasisi za kifedha kwa ajili ya kuwajengea elimu ya ujasiriamali, utafutaji masoko na uwekaji wa akiba wanufaika wa mikopo.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Manispaa, Mhe. Songoro Mnyonge amesema kuwa Halmashauri imeweza kutoa mikopo mingi kutokana na ukusanyaji mzuri wa mapato ya ndani jambo ambalo linapelekea ongezeko la fedha za mikopo na utoaji wa mikopo kwa wakati na amewaomba wananchi kuendelea kuwa wachangiaji wazuri wa mapato ya Serikali.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti tofauti baadhi ya wawakilishi wa vikundi hivyo wameipongeza Halmashauri kwa jitihada hizo na wameahidi kufanya kazi kwa bidii ili kuweza kufanya marejesho na kupata fursa ya kuweza kukopeshwa tena.
Katika mwaka wa fedha 2021/2022 Manispaa ya Kinondoni imeweza kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi za Kitanzania bilioni 6 na katika mwaka wa fedha 2022/2023 Manispaa inatarajia kutoa mikopo ya jumla ya shilingi za Kitanzania bilioni 4.6 ili kuwawezesha makundi maalum kuanzisha na kuendeleza shughuli zao za ujasiriamali zitakazowawezesha kujiongezea kipato na kushiriki kikamilifu katika ukuaji wa uchumi
Rai imeendelea kutolewa kwa watu wenye ulemavu kuchangamkia fursa kukopa ambapo marekebisho ya Kanuni ya mwaka 2021 yanaruhusu idadi ya wanaojiunga kwa watu wenye ulemavu ambapo hata mlemavu mmoja anaweza kuomba na kupatiwa mkopo.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.