Manispaa ya Kinondoni leo wameungana na Halmashauri nyingine kote nchini , kusherehekea kilele cha maadhimisho ya wiki ya Mazingira chenye kauli mbiu isemayo "Mkaa ni gharama, tumia nishati mmbadala ", kwa kuonesha bidhaa zao kupitia wajasiriamali waliowezeshwa yakilenga kuinua uchumi wa viwanda.
Katika maadhimisho hayo yaliyofanyika Kitaifa katika viwanja vya mnazi mmoja, jijini Dar es Salaam, ambapo mgeni rasmi wake akiwa Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh Samia Suluhu Hassan yalilenga kutoa elimu na uelewa juu ya utunzaji na Uthamini wa Mazingira, ambapo yalipambwa kwa burudani za kiasili pamoja na shughuli za ujasiriamali zilizokuwa zikioneshwa uwanjani hapo.
Katika hotuba yake Mama Samia suluhu amewataka watanzania kuelewa athari zitokanazo na ukataji wa miti kiholela na kuhakikisha wanakuwa walinzi wa kwanza wa Mazingira hayo.
Amezitaja athari hizo kuwa ni kukimbiza wanyama, kupoteza matunda ya asili, kuharibu makazi ya wadudu wenye kazi mbalimbali, kuharibu misitu inayotusaidia kunyonya joto au hewa ukaa na bahari kuingia eneo la makazi ya watu.
Naye Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Mazingira Mh. Januari Makamba alipokuwa akimkaribisha Makamu wa Rais amesema siku hii ambayo huadhimishwa 05/06 kila mwaka ni siku ya kuhakikisha uelewa unakuwepo kwa watanzania ya kwamba maendeleo huenda sambasamba na utunzaji wa mazingira hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kusimama kwenye nafasi yake kwa swala hilo.
Akitoa salamu za Mkoa wa Dar es salaam, Mkuu wa Mkoa huo Mh Paul Makonda amesema zipo changamoto zinazoukabili Mkoa wake, na kuzianisha kuwa ni swala la mafuriko, pamoja na uchafu uliokithiri na kutangaza tarehe 01/07/2018 kuwa siku maalumu ya operesheni ya usafi kwenye Mkoa wake.
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa vyama na Serikali ,watumishi kutoka Halmashauri za Mkoa wa Dar es salaam pamoja na mikoa ya jirani, yaliyoenda sambamba uoneshaji wa bidhaa za wajasiriamali pamoja na utoaji wa tuzo za ushindi wa utunzaji wa Mazingira.
Imeandaliwa na
Kitengo cha Uhusiano Manispaa ya Kinondoni
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.