Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni leo imetoa tuzo, vyeti pamoja na fedha taslimu kwa wakuu wa shule, waalimu wa masomo pamoja na Kata zilizofanya vizuri katika ufaulu wa matokeo ya mtihani wa darasa la saba kwa mwaka 2017.
Tuzo hizo zimetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh Alli Hapi alipokuwa mgeni rasmi katika tafrija za kuwapongeza waalimu hao zilizofanyika katika viwanja vya shule ya Msingi mbuyuni.
Amesema tuzo hizi ni kutokana na matokeo mazuri ya ufaulu kwa mwaka huu ambapo yameiweka Kinondoni katika kilele cha Taifa na hii ni kuonyesha ushirikiano, juhudi, maarifa na weledi wa waalimu wetu pamoja na viongozi wetu.
"Matokeo ya mwaka huu yametuweka katika kilele chá Taifa, rekodi hii iliyotokea mwaka huu, ama haijawahi kutokea kabisa , tumevunja rekodi katika historia ya Wilaya na Manispaa ya Kinondoni, Jambo hili sio Jambo la kubeza kwa sababu linatasfiri juhudi, ushirikiano na kazi kubwa ambayo viongozi wetu wameifanya. "Amesema Hapi
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Mh Benjamin sitta amesema lengo ni kutaka watanzania waelewe umuhimu na faida ya Elimu bure iliyosaidia kupunguza utoro, hali iliyopelekea wanafunzi wote kuhudhuria vipindi na kufanya mitihani kwa umakini.
Ameongeza kuwa lengo pia ni kuwapa moyo na kuthamini kazi nzuri na mchango wao mkubwa walioufanya katika kuhakikisha Kinondoni inaibuka kidedea katika ufaulu wa matokeo ya mtihani wa darasa la saba kwa mwaka 2017.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Ndg Aron Kagurumjuli ameainisha makundi yaliyopata tuzo hizo pamoja na zawadi kuwa ni walimu wakuu wa shule 78, zenye ufaulu zaidi, shule 10 zenye mabadiliko makubwa zaidi katika ufaulu, waalimu waliofundisha kikamilifu na kwa weledi na kutoa "A" nyingi kwenye masomo yao pamoja na kata zilizofanya vizuri.
Ameongeza kuwa Kinondoni imedhamiria na imejipanga kuelekea 2018, inashikilia rekodi hii kwa kufanya kazi kwa umakini na weledi mkubwa kwani ndiyo nguzo na silaha ya mafanikio.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh Alli Hapi amewataka waalimu kuhakikisha wanaendeleza juhudi hizo ili kufikia malengo mazuri na makubwa katika sekta ya elimu kwani ndio ufunguo wa maisha.
Tafrija hii imehudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo Baraza la madiwani, wenyeviti wa Serikali za Mitaa, wawakilishi kutoka Bank ya NMB pamoja na wakuu wa idara na vitengo wa Manispaa ya Kinondoni.
Imetolewa na
Kitengo cha Uhusiano na Habari
Manispaa ya Kinondoni
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.