NI KWA KUSHIRIKIANA NA SHIRIKA LISILO LA KISERIKALI LA JHPIEGO CHINI YA MPANGO WA "TUPANGE PAMOJA" LENYE OFISI ZAKE MIKOCHENI.
Manispaa ya Kinondoni
kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la JHPIEGO chini ya mpango wa "Tupange pamoja" wametoa semina elekezi kwa kata kumi kati ya kata ishirini za Manispaa hiyo,juu ya umuhimu wa njia sahihi za uzazi wa mpango, walengwa wakiwa ni kinamama na wanawake wajawazito.
Akiongea wakati wa zoezi hilo, mratibu wa huduma za afya ya uzazi Baba, Mama na mtoto kinondoni Bi Edith Mboga amesema wameamua kutoa elimu hiyo lengo ikiwa ni kuongeza uelewa wa matumizi ya njia hizi kwa wananchi ili waweze kupanga uzazi ulio bora na salama.
Akitoa takwimu za utumiaji wa njia hizo kwa Manispaa ya Kinondoni Bi Edith Mboga amesema kiwango kimeshuka kwani kitaifa inatakiwa kufikia asilimia 32, na kwa sasa kiwango kilichofikiwa cha matumizi hayo ni 11.4.
Akifafanua hilo amesema ndio maana wameamua kusogeza huduma hizi kwa karibu na wananchi ili waweze kupatiwa kwa usahihi, kwa wakati na kwa uelewa utakaomfanya mwananchi kuchagua njia ipi iliyobora zaidi.
Amezitaja njia hizo kuwa ni matumizi ya condom, sindano, vidonge, vijiti na vipandikizi.
Aidha huduma nyingine zinazotolewa katika semina hiyo ni pamoja na Upimaji wa hiari wa virusi vya UKIMWI, Upimaji wa saratani ya shingo ya kizazi, shinikizo la damu pamoja na chanjo kwa watoto chini ya miaka 5.
Zoezi hilo la siku tatu katika kila Kata, limeanzia kata ya Hananasifu, na linatarajiwa kuendelea katika Kata ya Tandale, Mwananyamala, Kigogo, Wazo, Ndugumbi, Tegeta, Salasala, Bunju na Kawe.
Imeandaliwa na
Kitengo Cha Habari na Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.