Manispaa ya kinondoni katika kuadhimisha siku ya wazee duniani yenye kauli mbiu isemyao"Wazee ni hazina ya Taifa, tuenzi juhudi za kutetea haki na ustawi wao", imegawa vitambulisho takribani 900 vya matibabu kwa wazee, pamoja na kutoa huduma za vipimo vya afya kwa magonjwa yasiyoambukiza kwa wazee wasiopungua 600, zoezi lililofanyika katika viwanja vya Mwinjuma CCM.
Akigawa vitambulisho hivyo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Katibu Tawala ya Wilaya hiyo Bi.Stella Msofe amesema, Serikali inajivunia kuwa na wazee kwani ndiko hazina kubwa ya busara na mafunzo katika kutekeleza majukumu ya Serikali inapatikana.
"Wazee ni hazina kubwa na sisi kama Serikali tunajivunia kuwa nanyi, hivyo jukumu letu kubwa ni kuhakikisha mnatimiziwa haki yenu ya msingi ambayo ni huduma za afya zilizo bora bila usumbufu" Amesema Katibu tawala.
Akitoa taarifa ya huduma kwa wazee katika Manispaa ya Kinondoni kwenye maadhimisho hayo, Mganga Mkuu wa Manispaa hiyo, Dr.Festo Dugange amesema Manispaa ya Kinondoni imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutekeleza Sera ya wazee ya Wizara ya Afya kwa kuboresha huduma za afya kwa wazee,ikiwemo utoaji wa vitambulisho vya matibabu.
Ameongeza kuwa kwa kutambua umuhimu wa siku ya wazee, na kutekeleza kauli mbiu ya mwaka huu, huduma mbalimbali zimetolewa katika maadhimisho hayo ambazo ni kujiandikisha na kutoa vitambulisho vya wazee, kupima uzito na urefu, kusoma BMI, vipimo vya maabara, kupima malaria na kupima macho.
Huduma nyingine ni kupima tezi dume kwa kutumia damu, ushauri wa VVU, ushauri kuhusu maambukizi ya TB/Ukoma, na ushauri kuhusu lishe.
Maadhimisho hayo yaliyofanyika katika viwanja vya Mwinjuma CCM, pia yalienda sambamba na burudani pamoja na michezo ya kufukuza kuku kwa wazee wanawake na wanaume, kuvuta kamba pamoja na burudani ya miziki ya zamani.
Imeandaliwa na
Kitengo cha habari na Uhusiano.
Manispaa ya kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.