Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, katika utekelezaji wa sera na maelekezo ya Wizara ya Afya maendeleo ya Jamii Jinsia wazee na watoto na OR-TAMISEMI imesaini mkataba wa lishe utakaotumika kutekeleza mapango jumuishi wa lishe wa Kitaifa(NMNAP) wa mwaka 2016-2017/2021, kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
Akisaini mkataba huo kati yake na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh.Daniel Chongolo, Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Ndg Aron Kagurumjuli amesema Manispaa yake iko tayari na imejipanga vizuri kuanza ukurasa mpya wa utekelezaji wa afua za lishe kwa ufanisi na kwa vitendo, na kwa kuzingatia mahitaji ya mkataba huo, kwani kwa kufanya hivyo itakua imeenda sambamba na uboreshaji wa afya ya mtoto mwenye umri chini ya miaka mitano, kwa kumpatia lishe bora na yenye afya kwa mujibu wa miongozo, sera, na kanuni katika kufikisha tija inayokusudiwa.
Akifafanua mahitaji yaliyoko katika sera hiyo ya lishe, Mganga Mkuu wa Manispaa hiyo Dkt. Festo Dugange amesema Sera hiyo inasisitiza kila Halmashauri kutenga bajeti ya kiasi cha tsh 1000/=kwa kila mtoto wa umri chini ya miaka 5, kutoka mapato ya ndani, kwa lengo la kutekeleza shughuli za lishe kwenye maeneo ya kipaumbele.
Ameyataja maeneo hayo ya kipaumbele kuwa ni watoto kupata vyakula vyenye virutubisho sahihi na kwa kiasi kinachostahili, kuhakikisha elimu ya lishe inatolewa kikamilifu kwa wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano, kuhakikisha watoto wenye utapiamlo mkali wanapatiwa matibabu stahiki, na kufanya kaguzi za vyakula hasa chumvi zenye madini joto.
Nyingine ni kuhakikisha wajawazito wanapatiwa madini chuma na vidonge vya Foliki Acid ili kuzuia upungufu wa damu na matatizo yanayosababishwa na ukosefu wa madini hayo kwa watoto, kutekeleza vikao vya Halmashauri vya kamati ya lishe kila robo kwa lengo la kufanya tathmini ya hali ya lishe na kuhakikisha wanashirikiana na wadau mbalimbali wa lishe walioko katika Halmashauri kwa lengo la kufanikisha.
Hafla hiyo ya kutiliana saini mkataba huo iliyofanyika katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya, imehudhuriwa pia na Katibu tawala wa Wilaya hiyo Bi. Stella Msofe, na Afisa lishe wa Manispaa hiyo Bi. Emiliana Sumaye
Imeandaliwa na
Kitengo cha Uhusiano na Habari.
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.