Akipokea mifuko hiyo ya cementi kutoka kanisa la Inuka uangaze linaloongozwa na Mtume Boniface Mwamposa, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh.Daniel Chongolo amesema imekuja wakati muafaka kwani itasaidia kuleta hamasa ya nguvu ya wananchi katika kuhakikisha kunakuwepo na mafanikio ya utatuzi wa changamoto kubwa ya madarasa iliyoko Wilayani hapo.
Amesema Serikali ya awamu ya tano dhamira yake kuu ni kuboresha miundombinu ya elimu pamoja na mfumo wake, hivyo mifuko hiyo imekuja kipindi ambacho Wilaya yake imepanga kufikia mwezi wa tatu mwaka huu iwe imekamilisha madarasa mia moja.
"Tunamshukuru na kumpongeza Mchungaji na Mtume Mwamposa pamoja na kanisa lake lote, kuona umuhimu wa kuchangia swala la elimu, niseme tu kwamba Msaada huu wa mifuko ya cement umekuja wakati mwafaka, kwani tulishajiwekea malengo mkakati ya kutatua changamoto iliyopo mbele yetu ya vyumba vya madarasa kwa kushirikiana na nguvu za wananchi kuhakikisha tunajenga mdarasa mia moja ifikapo mwezi wa tatu, ikiwa ni hatua za awali za kuhakikisha tunakabiliana na upungufu wa vyumba vya madarasa katika Wilaya yetu.".Amebainisha Chongolo
Ameongeza kuwa Jamii yetu inajengwa na taasisi mbalimbali ambazo kwa pamoja zikishirikiana na serikali zitaleta Matokeo chanya, hivyo tukio la leo limedhihirisha nia thabiti mliyonayo ya kumuunga mkono Mh. Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli ya kuboresha miundombinu ya elimu Nchini.
Akikabidhi mifuko hiyo, Mchungaji na Mtume Boniface Mwamposa amesema ni katika kuunga mkono juhudi za Mh Rais katika kuboresha sekta ya Elimu, kadhalika ni kutekeleza agizo la Mungu, kwani hata biblia imeandika katika kitabu cha Mithali 4:13 kuwa "mkamate sana elimu, usimwache aende zake mshike, maana yeye ndo uzima wako" na kuahidi kuendelea kusaidia swala zima la elimu pale inapopasa.
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni Mhe Benjamin Sitta katika kushuhudia ugawaji huo wa mifuko ya cement ameupongeza uongozi mzima wa kanisa hilo kwa azma njema waliyonayo katika elimu, na kuzihamasisha taasisi nyingine kufanya hivyo ili kuleta tija katika sekta hii Muhimu ya Elimu katika Taifa letu.
Imeandaliwa na
Kitengo Cha Habari na Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.