NI KATIKA KUADHIMISHA SIKU YA MKULIMA YENYE LENGO LA KUMPATIA MDAU WA SEKTA HIYO ELIMU NA MBINU BORA ZA KILIMO CHENYE FAIDA.
Manispaa ya Kinondoni imekutanisha wadau zaidi ya 400, kwa lengo la kujadili mikakati madhubuti ya kuboresha sekta ya kilimo, ikiwa ni katika kuadhimisha siku ya mkulima, hafla iliyofanyika katika Kituo cha kilimo Malolo, Kata ya Mabwepande.
Maadhimisho hayo yaliyohusisha wakulima, wafugaji, wasindikaji wa vyakula, wadau wauzaji wa pembejeo pamoja na wadau mbalimbali wa masuala ya Kilimo, yalilenga kuwakutanisha ili kuweza kubadilishana uzoefu wa mbinu bora za kilimo, ikiwa ni pamoja na kutambua umuhimu wa mnyororo wa thamani katika matumizi na upatikanaji wa pembejeo bora za kilimo.
Akiongea katika maadhimisho hayo, Afisa Kilimo wa Manispaa Ndg. Salehe Hija amesema, siku hii ni muhimu kwa wadau wa sekta nzima ya kilimo kukutana na kupeana mbinu si tu za mafanikio, bali pia njia mbadala za kukabiliana na changamoto zinazowakabili.
"Kwa Manispaa ya Kinondoni, Kituo cha Malolo ndio sehemu sahihi ya wadau wetu kukutana na kubadilishana uzoefu, kwani wataalam wote wapo, na pia ni rahisi kufikika na watu wengi, tofauti na maonesho ya wakulima nane nane na ikizingatiwa sasa tuko kwenye teknolojia ya Kilimo cha kisasa mijini. Ni rahisi kuwafundisha mbinu mpya za kilimo hapa Malolo ili nao waweze kuzitumia" Amesema Hija.
Katika maadhimisho hayo pia kulitolewa mafunzo ya ufugaji wa samaki, jinsi ya kuchagua mbegu bora za kilimo, usindikaji wa mazao ya kilimo pamoja na mafunzo ya uhifadhi salama wa chakula.
Maadhimisho hayo pia yamehudhuriwa na wadau mbalimbali kama vile mfuko wa pembejeo, bima ya kilimo na wamiliki wa maduka yanayosambaza pembejeo za kilimo.
Imeandaliwa na ,
Kitengo cha Habari na Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.