Manispaa ya Kinondoni imekabidhiwa Maktaba ya kisasa yenye thamani ya zaidi ya milioni themanini kutoka Korea ya Kusini kwa lengo la kuimarisha mfumo wa Elimu kwa shule za msingi utakaowajengea wanafunzi Utamaduni wa kusoma.
Maktaba hiyo imepokelewa leo na Mstahiki Meya Manispaa Kinondoni Mh Benjamin Sitta katika tafrija iliyofanyika kwenye viwanja vya shule Msingi Bongoyo .
Akipokea maktaba hiyo Meya Sitta amesema anafurahishwa zaidi kuona tunapiga hatua katika mfumo mzima wa elimu kwa kuwa na maktaba ya kisasa inayotumia mifumo ya kiteknolojia kitu ambacho kitamjengea mtoto utamaduni wa kupenda kusoma.
"Nimefurahi Sana kwasababu library hii ni ya kisasa unaweza kuona mandhari yake ni nzuri, wameenda kiteknolojia zaidi "amesisitiza Meya.
Aidha amemshukuru Balozi wa Korea ya kusini kwa kuona umuhimu wa kuwekeza katika Elimu kitu ambacho kitamkuza mtoto na kumfanya kuwa na Utamaduni wa kusoma.
Naye Balozi wa Korea ya Kusini nchini Tanzania Ndg Keum Young Song amesema Serikali yake itaendelea kusaidia miradi ya ujenzi wa maktaba ndogo kwa shule za Msingi ili iweze kusaidia wanafunzi kusoma vitabu vya kiada na ziada kwa lengo la kupata misingi mizuri katika elimu.
Akifafanua umuhimu wa maktaba kwa wanafunzi Afisa Elimu Msingi Manispaa ya Kinondoni Ngd Kiduma Mageni amesema Maktaba ndio eneo pekee ambalo mwanafunzi anaweza kuwa na utulivu katika kusoma na kutafakari kwa kina bila kusumbuliwa na mtu yeyote.
Amesema Kinondoni inao mpango madhubuti wa kuziboresha shule zake kwa maana ya nyenzo za kufundishia pamoja na Mazingira rafiki ya kusomea yatakayomwezesha mwanafunzi kujenga utamaduni wa kujisomea na hasa ikizingatiwa maktaba hii ni ya kisasa kabisa yenye vifaa vyote vinavyohitajika kwa mwanfunzi kusoma bila malipo ya aina yeyote.
"Sisi Kinondoni tunataka tuoneshe mfano kwa vitendo, kwa kuunga mkono juhudi za Mh Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania za kutoa elimu bila malipo, tunashule kumi na tano, hii ni mojawapo, ambazo tunataka ziwe za kwanza kwa kipindi cha mwaka 2015 hadi 2020, ziwe shule zaidi ya shule zisizokuwa za Kiserikali "Ameongeza Mageni
Akizitaja changamoto za shuleni hapo, Mwalimu Mkuu wa shule ya Bongoyo Bi Alice Martine amesema shule hiyo inakabiliwa na uhaba wa nyumba za waalimu, miundombinu ya maji kwenye vyoo, miundo mbinu ya umeme, na Samani za ofisi.
Korea Kusini imetimiza miaka ishirini na tano ya urafiki kati yake na Nchi ya Tanzania na hadi kufikia leo kwa mujibu wa taarifa iliyosomwa kwetu na Balozi Keum Young Song imesema mpaka sasa imeshajenga jumla ya maktaba ndogo kumi na moja kwenye shule za msingi hapa Tanzania.
Imetolewa na
Kitengo cha Uhusiano.
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.