Manispaa ya Kinondoni imekabidhiwa hati ya manunuzi ya jengo la kilichokuwa kituo cha kulelea watoto yatima (Dogodogo Centre) yenye thamani ya takribani shilingi milioni 400, kwa lengo la kubadilisha matumizi na kuwa kituo cha Afya.
Hati hiyo imekabidhiwa leo kwa Mstahiki Meya Manispaa ya Kinondoni Mh Benjamin Sitta ikishuhudiwa na kamati ya Fedha na Uongozi, pamoja na wananchi, hafla iliyofanyika katika Kata ya Kigogo, eneo lililopo jengo hilo.
Akipokea hati hiyo Meya Sitta amesema ununuzi wa jengo hilo ni katika kutekeleza mkakati wa Manispaa wa kuhakikisha huduma za Afya zinaboreshwa kwa kiwango kikubwa na kuhakikisha wananchi wanapatiwa huduma bila usumbufu wowote, kwani Serikali ya awamu ya tano ni Serikali ya viwanda hivyo inahitaji kujengwa na wananchi wenye Afya bora.
Ameongeza kuwa azma ya Manispaa ni kuhakikisha inaondokana na msongamano wa wagonjwa kwani hapo awali zahanati ya kigogo ilikuwa inapokea idadi kubwa ya wagonjwa ikilinganishwa na uwezo wa miundombinu iliyopo, kadhalika kuleta usumbufu usio wa lazima.
Naye Mganga Mkuu wa Manispaa hiyo Dkt Festo Dugange amesema kuwa Manispaa ya Kinondoni imejipanga kikamilifu kuboresha miundombinu katika sekta ya Afya kwa wakazi wake, ili waweze kupatiwa matibabu yanayokidhi viwango kwa wakati na ubora unaostahili.
Akiongea mara baada ya kukabidhi hati hiyo, mratibu wa kituo cha Dogodogo centre Bw. Sabas Massawe amesema wamefarijika kukabidhi jengo hilo kwa Manispaa ya Kinondoni kwani wanaamini huduma za Afya zitakazotolewa hapo zitakuwa msaada mkubwa kwa wananchi.
Imetolewa na
Kitengo cha Habari na Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.