Manispaa ya Kinondoni leo imekabidhiwa gari aina ya Ford transit chasis namba WFOLXXTTFL5U480355 kutoka kwa mamlaka ya mapato Tanzania(TRA) kwa ajili ya huduma za afya kituo cha Afya Magomeni.
Akikabidhi gari hilo Mkurugenzi wa idara ya Elimu kwa mlipakodi mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Ndg Richard Kayombo amesema ni kutokana na maombi yaliyoletwa kwao na Kamati ya bodi ya kituo hicho yakionesha uhitaji uliopo wa gari hilo la kubebea wagonjwa katika kituo hicho.
Amesema TRA inayo dhamira ya dhati kabisa ya kuona huduma za afya nchini zinaimarika na ndio maana imetoa gari hilo kwa Manispaa hiyo na kuwataka litumike kwa shughuli husika na si vinginevyo.
"Gari hili lilikuwa limehifadhiwa kwenye bandari kavu ya Ubungo na pia lilikuwa kwenye orodha ya magari yanayotakiwa kunadiwa, lakini kwa kutambua umuhimu wa ubora wa huduma za afya, tunalikabidhi kwenu ili likanyanyue na kusogeza huduma hizo katika hali inayoridhisha, ni imani yangu litatumika kwa matumizi hayo "Amesisitiza Kayombo.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Bi Patricia Henjewele ameishukuru mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) kwa ufadhili wa gari hilo, na kuahidi kulitunza na kutumika kwa matumizi yaliyokusudiwa.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa kamati ya bodi ya kituo cha Afya cha Magomeni Ndg Iddi Msumagila ameishukuru TRA kwa ufadhili wa gari hilo na amesema litasaidia kupunguza adha iliyokuwepo ya ukosekanaji wa gari ya Ambulance pale inapotakiwa kumpeleka mgonjwa katika hospital ya rufaa kwa matibabu zaidi.
Imetolewa na
Kitengo cha Uhusiano na Habari
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.